Serikali yaanika mambo 10 sekta binafsi

Katibu mkuu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Profesa Elisante ole Gabriel

Muktasari:

  • Akizungumza na Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF), katibu mkuu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Profesa Elisante ole Gabriel alisema kuwa sekta binafsi inapaswa kufuata sheria za nchi na uwekezaji, kulipa kodi kwa wakati, kuwa na mfumo rafiki wa mawasiliano na kujisafisha kibiashara kupitia machapisho ya ukaguzi wa hesabu.

        Alfred Zacharia na Halili Letea [email protected]

Dar es Salaam. Serikali imetaja mambo 10 ambayo sekta binafsi inapaswa kufanya ili kuaminika kiutendaji na kibiashara.

Akizungumza na Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF), katibu mkuu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Profesa Elisante ole Gabriel alisema kuwa sekta binafsi inapaswa kufuata sheria za nchi na uwekezaji, kulipa kodi kwa wakati, kuwa na mfumo rafiki wa mawasiliano na kujisafisha kibiashara kupitia machapisho ya ukaguzi wa hesabu.

Pia, inapaswa kuwa na mipango thabiti ya biashara, kuzingatia mnyororo wa thamani katika biashara, utamaduni wa kufanya kazi, kuboresha viwanda vya huduma, kukuza mvuto wa viwanda na kuboresha huduma maeneo ya viwanda.

Mkurugenzi wa sera wa TPSF, Gilead Teri alitoa ombi kwa Serikali kusitisha mpango wa kufunga baadhi ya viwanda.

“Ni vyema Serikali ijikite katika kuwawezesha wawekezaji ili waweze kumudu uendeshaji wa viwanda vyao kuliko kuwatishia kuvifunga,” alisema.

Hata hivyo, Ole Gabriel alilitupilia mbali ombi hilo akisema suala hilo lipo kisheria.

“Ikiwa kiwanda kitafuata na kukamilisha taratibu zote za nchi na makubaliano ya kibiashara, hakuna Serikali itakayo weza kukifungia, lakini kama kitashindwa, hatuwezi kukiacha,” alisisitiza.