Serikali yatenga Sh155 bilioni kujenga maghala mapya

Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage (kushoto), Katibu wa Bodi ya Baraza la Nafaka la Ukanda wa Afrika Mashariki (EAGC), Gerald Masila (katikati) na mwenyekiti wa bodi hiyo, Eugene Rwibasira (kulia) wakionyesha vitabu vya mpango mkakati wa tatu wa mwaka 2018 hadi 2022 baada ya kuuzindua jijini Dar es Salaam juzi. Picha na Ericky Boniphace

Muktasari:

Mpango huo ulibainjishwa juzi na Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage kwenye mkutano wa mwaka wa Baraza la Nafaka Ukanda wa Afrika Mashariki (EAGC) uliozindua mpango mkakati wa miaka mitano (2018-2022) kwa lengo la kukuza biashara ya nafaka katika eneo hilo.

Dar es Salaam. Ili kukabiliana na upungufu unaoweza kujitokeza, Serikali inatarajia kutumia Sh155.1 bilioni kujenga maghala ya kuhifadhi chakula maeneo mbalimbali nchini.

Mpango huo ulibainjishwa juzi na Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage kwenye mkutano wa mwaka wa Baraza la Nafaka Ukanda wa Afrika Mashariki (EAGC) uliozindua mpango mkakati wa miaka mitano (2018-2022) kwa lengo la kukuza biashara ya nafaka katika eneo hilo.

Majibu ya Mwijage yalitokana na kuwapo kwa hoja kuwa kuna changamoto ya upatikanaji vibali vya kusafirisha nafaka kwenda nje ya nchi, wakati mwingine kibali kinaweza kusitishwa kabla zabuni ya mfanyabiashara haijakamilika.

“Suala la vibali vya kusafirisha nafaka linasababishwa na kutokuwa na uhakika wa kiwango cha chakula kinachokuwapo nchini. Kulikuwa na hofu ya hazina ya chakula, lakini tuna mpango wa kujenga maghala makubwa zaidi hivyo mambo ya vibali hayatakuwepo tena,” alisema Mwijage.

Licha ya kutofafanua idadi ya maghala hayo, uwezo wa kuhifadhi na chanzo cha fedha hizo, Mwijage alisema mojawapo litazinduliwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wiki ijayo mkoani Dodoma na kubainisha maeneo mengine yatakapojengwa kuwa ni Makambako, Katavi na sehemu nyingine zenye uhitaji.

“Baada ya ujenzi wa magahala hayo, Serikali itakuwa na jukumu moja tu, kusimamia bei na kuhakikisha wakulima wanapata soko la mazao yao kwa urahisi zaidi,” alisema Mwijage.

Awali, akifungua mkutano huo mwenyekiti wa EAGC, Eugene Rwibasira alisema licha ya changamoto ya usafirishaji iliyopo, mpango mkakati uliozinduliwa utasaidia kuongeza ujazilishaji nafaka na biashara ya mazao hayo na ubora wake sokoni. “Tatizo kubwa la biashara ya nafaka katika ukanda huu ni sisi wenyewe kutouziana biashara ndani ya ukanda, ni ndogo kuliko mabara mengine. Kwa Tanzania kuna tatizo la vibali vya usafirishaji,” alisema.