Sukari ya Zanzibar yazuiwa kuuzwa bara

Muktasari:

  • Kiwanda cha Sukari cha Zanzibar kimeongeza uzalishaji

Licha ya kuwapo hasama ya kukuza viwanda nchini, Kiwanda cha Sukari cha Zanzibar kimenyimwa kibali cha kuuza zaidi ya tani 3,000 ya bidhaa hiyo upande wa bara.

Meneja biashara wa kiwanda hicho, Pranav Shah alisema wameshindwa kuuza sukari hiyo Zanzibar kwa sababu wanapata hasara ya Sh18,000 kwa kila mfuko wa kilo 50 wakitoa gharama za uzalishaji.

“Tunataka soko la bara kwa sababu ya tofauti ya bei iliyopo. Hapa tunauza mfuko wa kilo 50 kwa Sh65,000 hadi Sh70,000 wakati Dar es Salaam inauzwa Sh115,000.

“Tunazo tani 3,000 tulizozalisha tangu Januari, tumeshindwa kuuza kuepuka hasara. Kuuza bara tunahitaji kibali ambacho hatujapata mpaka sasa,” alisema Shah.

Alifafanua kuwa uagizaji wa sukari kutoka nje inayouzwa kwa bei ndogo ni changamoto kwao.

Mkurugenzi mtendaji wa kampuni hiyo, Vicky Patel alisema kiwanda kimeongeza uzalishaji ikiwa ni pamoja na kuingia mkataba wa kununua miwa ya wakulima 500.

Waziri wa Viwanda, Biashara na Masoko wa Zanzibar, Balozi Amina Salum Ali alisema Serikali inaweka mikakati ya kuondoa changamoto zilizopo.

“Suala kubwa hapa ni bei wanayouzia Zanzibar ni ndogo ukilinganisha na gharama wanazotumia kuzalisha. Tutaangalia gharama zao, kodi na kuweka sawa,” alisema Balozi Amina.

Mahitaji ya sukari Tanzania ni tani 590,000 ambazo kati yake tani 420,000 hutumika viwandani na tani 170,000 katika mahitaji ya nyumbani kwa mwaka.

Hata hivyo, uwezo wa uzalishaji wa viwanda vya ndani ni tani 300,000 hivyo kuwa na upungufu wa tani 290,000 kila mwaka. Kutokana na upungufu huo, kiasi kinachokosekana huagizwa kutoka nje.

Waziri wa Biashara, Viwanda na Uwekezaji, Charles Mwijage hakuwa tayari kuzungumzia suala hilo akisema anaandaa taarifa kwa ajili ya kikao cha Baraza la Mawaziri.

“Siwezi kuongea chochote, niko na wataalamu wangu tunaandaa taarifa kwa ajili ya kikao cha ‘cabinet’,” alisema Waziri Mwijage.