Sukari ya viwandani yazuia bidhaa za Kenya

Muktasari:

  • Ingawa soko la pamoja linaruhusu uhuru wa bidhaa, rasilimali watu na mtaji lakini bidhaa kama pipi, chokuleti na ice cream kutoka Kenya taarifa zinasema hutozwa kodi ya asilimia 25 zinapoingizwa Tanzania na Uganda kwa maelezo kuwa zinatumia sukari ya viwandani kutoka nje.

Licha ya kuwa na soko la pamoja kwa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki, wafanyabiashara wa Kenya wamelalamika bidhaa zao kutozwa ushuru zikiingia Tanzania na Uganda.

Ingawa soko la pamoja linaruhusu uhuru wa bidhaa, rasilimali watu na mtaji lakini bidhaa kama pipi, chokuleti na ice cream kutoka Kenya taarifa zinasema hutozwa kodi ya asilimia 25 zinapoingizwa Tanzania na Uganda kwa maelezo kuwa zinatumia sukari ya viwandani kutoka nje.

Taarifa zilizoripotiwa na gazeti la Business Daily la nchini Kenya zinasema mamlaka za nchi hizo mbili zimekataa kuvikubali vyeti vya asili ya bidhaa (certificates of origin) vinavyotolewa na Mamlaka ya Mapato Kenya (KRA).

Ofisa mtendaji mkuu wa Chama cha Wenye Viwanda Kenya (Kam), Phyllis Wakiaga alinukuliwa akisema, “Kwa bidhaa zinazozalishwa ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki hazipaswi kutozwa ushuru. Hata washindani wetu ndani ya jumuiya wanategemea sukari ya viwandani kutoka nje.”

Ofisa huyo alisema nchi zote za jumuiya hazizalishi sukari ya viwandani, hivyo kulazimika kuiagiza kutoka nje kwa ajili ya uzalishaji wao. Hata hivyo, mamlaka za Tanzania na Uganda zinaona kama Kenya inatumia vibaya makubaliano yaliyopo kujinufaisha.

KRA ilisema bidhaa hizo hazistahili kutozwa ushuru ingawa baadhi ya malighafi zake zinaagizwa kutoka nje.

Msemaji wa KRA, Julius Kihara alisema ushuru huo haupaswi kutozwa kama kiwango kilichosafirishwa hazidi tani 20,000 za ujazo kwa kila aina. Mara kadhaa biashara kati ya Tanzani na Kenya zimekuwa zikikumbwa na vikwazo ambavyo mamlaka husika zimezishughulikia haraka.

Mkurugenzi wa elimu kwa walipakodi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Richard Kayombo alisema Kenya imekiuka makubaliano ya jumuiya katika uagizaji wa bidhaa.

Alisema yapo makubaliano ya kutoza ushuru sawa (common external tariff) kwa bidhaa zinazotoka nje jambo ambalo halitekelezwi na Kenya.

Msimamo huo wa TRA unatokana na tangazo la Serikali nchini Kenya lililotolewa Mei 12, 2017 likiwaruhusu wafanyabiashara kuagiza sukari na maziwa bila kulipa ushuru kutokana na baa la njaa lililokuwa likilikabili Taifa hilo lililosababishwa na ukame ulioikumba baadhi ya mikoa yake.

Tangazo hilo lilitoa msamaha huo kuanzia tarehe ya kutolewa kwake mpaka Julai 31, 2017 likiruhusu kuingiza tani 9,000 za maziwa ya unga na sukari isiyo na kikomo.