TBL yaimarisha mauzo na mtaji Soko la Hisa Dar

Muktasari:

Kwa wiki iliyoishia Septemba 22, mauzo yalifika Sh53.5 bilioni yakiongezeka kwa takriban mara 10 kutoka Sh5.4 bilioni yaliyopatikana wiki iliyoishia Septemba 15. Mauzo hayo yalichangiwa na ongezeko la hisa kutoka milioni mbili mpaka milioni 4.4 ndani ya muda huo.

Dar es Salaam. Licha ya kutangaza kushuka kwa faida yake kutokana na kupigwa marufuku kwa pombe za viroba, wawekezaji wameendelea kuwa na imani na hisa za Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) hivyo kuongoza kwa mauzo kwenye Soko la Hisa Dar es Salaam (DSE) wiki iliyoishia.

Kwa wiki iliyoishia Septemba 22, mauzo yalifika Sh53.5 bilioni yakiongezeka kwa takriban mara 10 kutoka Sh5.4 bilioni yaliyopatikana wiki iliyoishia Septemba 15. Mauzo hayo yalichangiwa na ongezeko la hisa kutoka milioni mbili mpaka milioni 4.4 ndani ya muda huo.

TBL ilikuwa kinara baada ya kuuza asilimia 99 ya hisa zote zilizonunuliwa sokoni hapo, ikifuatiwa na Kampuni ya Vodacom iliyouza asilimia 0.22 na Benki ya CRDB ikifunga pazia hilo kwa kuuza asilimia 0.09.

Licha ya kuchangia kwenye mauzo ya soko, TBL ilifanya hivyo kwenye ukubwa wa mtaji wa kampuni za ndani ulioongezeka kwa Sh27 milioni na kufika Sh9.67 trilioni wiki hiyo, kutokana na kupanda kwa bei ya hisa zake kwa asilimia 0.75 hivyo kuuzwa kwa Sh13,400 kila moja.

Meneja Mkuu wa Orbit Securities, Simon Juventus alisema wawekezaji wana imani na mipango ya muda mrefu ya kampuni hiyo ndiyo maana hawajakatishwa tamaa na mtikisiko mdogo uliotokea hivi karibuni.

“Wawekezaji wa muda mrefu huwa hawaangalii leo, bali kesho wakitumaini mazingira yataimarika,” alisema meneja huyo.

Kwenye taarifa zake za fedha zilizoishia Machi 31, kampuni hiyo ilitangaza kupungua kwa faida yake kwa asilimia 29 ikilinganishwa na ilivyokuwa kwa mwaka uliopita. Sababu za kupungua kwa faida hiyo, zilielezwa kuwa ni zuio la uuzaji viroba lililofanya ipate Sh161.44 bilioni.

Mwenendo wa soko kwa ujumla ulikuwa mzuri kwani ukubwa wa mtaji wa kampuni zilizoorodheshwa uliongezeka kwa Sh293 bilioni kutoka Sh20.2 trilioni uliokuwapo wiki iliyopita hadi Sh20.5 trilioni wiki jana. Ongezeko hilo lilielezwa kutokana na kupanda kwa bei za hisa za Kenya Airways kwa asilimia 20, Uchumi Supermarkets (USL) kwa asilimia 12.5 na Benki ya KCB asilimia tisa.