TBS: Watanzania kuweni mabalozi wa bidhaa bora

Muktasari:

  • Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Profesa Egid Mubofu alisema hayo alipokabidhi vyeti na leseni za kuthibitisha ubora kwa wazalishaji wa bidhaa mbalimbali zaidi ya 60.

Shirika la Viwango Tanzania (TBS), limewataka Watanzania kuwa mabalozi wa kudhibiti ubora wa bidhaa ili kuweka mazingira mazuri ya kukubalika kwenye soko la kimataifa.

Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Profesa Egid Mubofu alisema hayo alipokabidhi vyeti na leseni za kuthibitisha ubora kwa wazalishaji wa bidhaa mbalimbali zaidi ya 60.

Alisema watumiaji wana nafasi nzuri kudhibiti ubora, jukumu lililo chini ya taasisi yake.

“Tunajitahidi kufanya kila linalowezekana kuondokana na bidhaa zisizo na ubora. Wazalishaji mtusaidie na walaji tunawaomba muache kununua bidhaa zisizothibitishwa. Hatuwezi kupeleka bidhaa nje ya nchi ikiwa haina ubora, soko la kimataifa lina ushindani mkubwa,” alisema Profesa Mubofu.

Mpango wa Serikali ni kuhakikisha Tanzania inakuwa na uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025 huku sekta ya viwanda ikichangia walau asilimia 40 kwenye Pato la Taifa (GDP).

Endapo ndoto hiyo itatimizwa, Tanzania itakuwa inasafirisha bidhaa nyingi nje ya nchi.

Kwa sasa, saruji ni miongoni mwa bidhaa za viwandani inayokidhi mahitaji ya ndani na ziada kupelekwa nje ambako inashindana na inayotoka Brazil, Iran na mataifa mengine yaliyoendelea. Mwaka jana, tani milioni 7.6 zilizalishwa ingawa mahitaji ya ndani ni tani milioni 4.15 pekee.

Kaimu Mkurugenzi wa Kitengo cha Udhibiti Ubora, Ashura Kilewela alikumbusha kutofautisha nembo ya TBS na alama ya ubora kutokana na baadhi ya wazalishaji kuweka nembo ya shirika hilo kwenye bidhaa zao badala ya alama hiyo.

“Angalieni kwa umakini, alama ya ubora ina gurudumu peke yake lakini nembo ya TBS ambayo wengi mnaitumia pembeni ina maneno ya Tanzania Bureau of Standars,” alisema Ashura.