TRA yazifungia shule za Eckernforde

Thursday October 26 2017

 

By Raisa Said, Mwananchi [email protected]

Tanga. Shule mbili na vyuo viwili vinavyomilikiwa na Taasisi ya Elimu ya Eckernforde ya jijini hapa vimefungiwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Tanga kwa kile kilichoelezwa kuwa zinadaiwa kodi za mwaka 2012 hadi 2016.

Meneja wa TRA Mkoa wa Tanga, Masawa Masatu alisema mamlaka ya mapato imezifungia shule hizo pamoja na Chuo cha Eckenforde kwa kushindwa kulipa kodi kwa muda mrefu.

Meneja huyo alisema endapo watashindwa kulipa kodi mali zote za taasisi hiyo zitazitaifishwa na Serikali.

Hata hivyo, meneja huyo hakutaja kiasi cha fedha kinachodaiwa huku akitaja majengo ya taasisi hiyo yaliyofungiwa kuwa shule za msingi, sekondari, chuo kikuu na chuo cha ualimu.

Alisema kufungiwa kwa taasisi hiyo ni mwendelezo wa mamlaka hiyo kukusanya madeni kwa wadaiwa sugu.

Makamu Mkuu wa Chuo cha Eckernforde Profesa John Kiango alisema wameshindwa kulipa kodi kutokana na idadi ndogo ya wanafunzi hivyo kwa sasa mikakati yao ni kuhakikisha wanaongeza idadi kubwa ya wanafunzi jambo litakalowaongezea kipato kitakachowasaidia kulipa kodi kwa wakati.

Advertisement