TTB wageukia vivutio vya mambo ya kale kuongeza watalii nchini

Muktasari:

  • Mkoa wa Songwe unajiandaa kushiriki Siku ya Kimondo Duniani Juni 30 mwaka huu

Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) imejipanga kuvitangaza vivutio vya mambo ya kale kukuza na kuongeza idadi ya watalii wanaotembelea nchini.

Mkurugenzi wa masoko wa TTB, Ernest Mwamwaja alisema vivutio vya mambo ya kale kama vile kimondo (pichani) kilichopo Mbozi mkoani Songwe ni sehemu muhimu wa utalii.

“TTB tutatoa msukumo kutangaza mambo ya kale kuwavuta watalii wa ndani na nje kutembelea maeneo hayo,” alisema Mwamwaja.

Akizungumza katika ziara, ya watendaji wa bodi hiyo waliotembelea kimondo kilichopo Mbozi na kufanya mkutano na uongozi wa Mkoa wa Songwe ili kujadili namna bora ya kuvitangaza vivutio vya utalii, Mwamwaja alisema rasilimali hizo huvuta watalii na wageni wengi kutoka nje.

Alisema upo ulazima wa kutumia nguvu kutangaza mambo ya kale kwani yanatoa historia ya Taifa na tamaduni mbalimbali zilizopo nchini.

Kwa kuanzia, Mkoa wa Songwe unajiandaa kushiriki Siku ya Kimondo Duniani (Meteorite Day) Juni 30 mwaka huu.

Aliwataka watoa huduma za utalii hasa wenye hoteli, wasafirishaji na waongoza watalii kuandaa safari za kwenda Mbozi kuangalia mambo ya kale ikiwamo kimondo ili kutanua wigo kwa watalii kutembea vivutio tofauti vilivyopo nchini.

Mhifadhi Msaidizi wa Kituo cha Kimondo cha Mbozi, Musa Msojo alisema Tanzania imebarikiwa vivutio vingi hasa vya mambo ya kale kama kimondo hicho kilichogundulika mwaka 1930.

“Hii ni nafasi kwa Watanzania na wageni kutembelea kivutio hiki na kujua historia yake,” alisema Msojo.

Alisema idadi ya wanaotembelea kivutio hicho ni ndogo hivyo kuwaomba wadau kuendelea kukitangaza ili kuongeza watalii.