Tani sita za samaki zanaswa Sengerema

Baadhi ya samaki aina ya sangara waliokamatwa wakiwa wameanikwa katika Kijiji cha Kawekamo wilayani Sengerema mkoani Mwanza. Picha na Daniel Makaka

Muktasari:

Ilidaiwa kuwa samaki hao waliokutwa wameanikwa kijijini hapo walikuwa kwenye harakati za kupelekwa nje ya nchi kimagendo.

       Sengerema. Tani sita za shehena ya samaki wachanga na wazazi aina ya sangara yenye thamani ya Sh24 milioni imekamatwa juzi katika Kijiji cha Kawekamo, Kata ya Nyampande wilayani hapa mkoani Mwanza.

Ilidaiwa kuwa samaki hao waliokutwa wameanikwa kijijini hapo walikuwa kwenye harakati za kupelekwa nje ya nchi kimagendo.

Katibu Tawala Wilaya ya Sengerema, Alen Augustine alisema kazi ya kukamata shehena hiyo ilifanikiwa baada ya vyombo vya dola kupata taarifa kutoka kwa raia wema kuhusu mipango ya kusafirisha samaki hao kwenda nje ya nchi kinyume cha sheria.

“Katika zoezi hilo, pia tumefanikiwa kukamata nyavu 012 za kuvuli samaki zenye matundu ya nchi 4.5 na sita zenye thamani ya Sh22.9 milioni,” alisema Augustine.

Kaimu Ofisa Uvuvi, Halmashauri ya Sengerema, Benerdictor Magaonda aliahidi kuwa ofisi yake itaendelea kuwasaka na kuwatia mbaroni wote wanaojihusisha na uvuvi haramu na biashara ya samaki bila kuzingatia sheria.

Ofisa Mtendaji Kata ya Nyamapande, Wiliam Donart aliwaomba wananchi kushirikiana na Serikali katika mapambano dhidi ya uvuvi na biashara haramu ya samaki.

Alisema mapambano hayo yatasaidia kulinda rasilimali hiyo kwa faida ya vizazi vya sasa na vijavyo.