Tanzania kutoshiriki mkutano wa utalii, utamaduni Oman

Muktasari:

  • Utalii ni miongoni mwa sekta zinazoongoza kwa kuliingizia Taifa fedha za kigeni

Imeelezwa kuwa Tanzania haitashiriki mkutano wa kimataifa kujadili namna utalii na utamaduni wa mataifa mbalimbali unavyoweza kufanikisha utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo Endelevu (SDG) kabla ya mwaka 2030.

Mkutano huo wa pili ulioandaliwa na Shirika la Utalii Duniani (UNWTO) kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (Unesco), utafanyika Desemba 11 hadi 12 jijini Muscat, Oman.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Meja Jenerali Gaudence Milanzi alisema: “Hatutashiriki, hatuwezi kwenda kila mahali, gharama ni kubwa. Tumeshiriki mikutano kadhaa ya Unesco iliyofanyika Paris, Ufaransa na Poland ambayo ilikuwa muhimu zaidi.”

UNWTO imeuchagua mwaka huu kuwa wa utalii endelevu ikiwa ni sehemu ya fursa za viongozi wa Serikali kubadilishana uzoefu na kuingia makubaliano ya kimkakati katika utekelezaji wa malengo ya SDG.

Katibu Mkuu wa UNWTO, Taleb Rifai alisema kuutangaza utamaduni wa jamii zilizopo maeneo mbalimbali duniani ni jambo muhimu linaloongeza hamasa ya wananchi husika kulinda na kuuendeleza utalii huu.

Katika mkutano huo, mawaziri wa nchi husika watapata fursa ya kulinda na kuendeleza utamaduni na utalii wa maeneo ya urithi wa dunia.

Naibu Katibu Mkuu wa Unesco-Utamaduni, Francesco Bandarin alisema: “Utamaduni ni kiungo muhimu cha ustawi wa jamii. Kuunganisha utalii na utamaduni ni fursa nyeti ya ku fanikisha utekelezaji wa SDG.”

Utalii ni miongoni mwa sekta zinazoongoza kwa kuliingizia Taifa fedha za kigeni, licha ya vivutio lukuki vilivyopo nchini.

Mwaka jana Tanzania ilipokea takriban wageni milioni 1.7 na kuliingizia Taifa Sh4.6 trilioni.

Alipokuwa akizindua bodi ya wakurugenzi wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe alitaka kuvitangaza vivutio vilivyopo na kuhakikisha mpaka mwakani, idadi hiyo inafika milioni tatu.