Tuesday, October 10, 2017

Tanzania yakabiliwa uhaba wa magunia

 

By Daniel Mjema, Mwananchi dmjema@mwananchi.co.tz

Moshi. Tanzania inakabiliwa na uhaba mkubwa wa magunia ya katani yanayotumika kusafirishia kahawa iliyokobolewa nje ya nchi.

Uhaba huo unaelezwa kutokana na kusimamishwa ghafla kwa uzalishaji msimu wa 2017/18 na Kampuni ya Mohammed Enterprises (MeTL), ambayo ni mzalishaji pekee.

Ofisa Mwandamizi wa MeTL anayeshughulikia uzalishaji wa magunia, Ndekirwa Nyari alikiri kuwapo upungufu huo lakini akabainisha kuwa uzalishaji unakwenda kwa kasi na tatizo hilo litakuwa historia. “Tumeanza uzalishaji wiki hii, kuanzia wiki ijayo tatizo hili litabaki kuwa historia. Uzalishaji ulikuwa haukidhi mahitaji ingawa tuliendelea kusambaza magunia,” alisema Nyari.

Alisema amekuwa akipokea simu nyingi kutoka mikoa inayolima kahawa nchini wakitaka magunia hayo na tayari wameanza utekelezaji wa maombi hayo. Alisema tayari amepeleka marobota 12 sawa na magunia 2,400 mjini Moshi.

Takwimu zinaonyesha sekta ya kahawa inahitaji kati ya magunia 800,000 na milioni moja kila msimu, hivyo uhaba uliojitokeza ulisababisha wasafirishaji kuyaagiza nje ya nchi. Kutokana na uhaba uliopo, kwenye msimu wa mwaka 2016/17, baadhi ya wakulima walinunua magunia aina ya jute yanayotengenezwa Bangladesh na India.

Taarifa zinaeleza kuwa MeTL ilipunguza uzalishaji baada ya wadau wa kahawa kupitisha azimio mwaka 2013 linaloiagiza Bodi ya Kahawa Tanzania (TCB) kuruhusu matumizi ya magunia mbadala.

Naye Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TCB, Primus Kimaryo alikiri kuwapo kwa uhaba wa magunia hayo na kwamba, msimu wa 2017/18, MeTL ilisimamisha ghafla uzalishaji.

“Utaratibu ni kuwa tunapoanza msimu viwanda vinapeleka order.Walipopeleka akasema amesimamisha uzalishaji,” alisema.

Kimaryo alisema bodi iliwasiliana na Bodi ya Katani Tanzania (TSB), kujua kama wapo wazalishaji wengine wenye uwezo lakini ilionekana ipo haja ya kuagiza kutoka nje.

-->