Uagizaji wa bidhaa kutoka Tanzania waongezeka Kenya

Muktasari:

  • Tanzania ni muuzaji wa nne mkubwa wa bidhaa zake nchini Kenya

Nairobi. Wakati uuzaji wa bidhaa za Kenya ukishuka kwa takriban asilimia 19 ndani ya miezi 10, uagizaji wa bidhaa za Tanzania umeongezeka kwa asilimia 25.44.

Kati ya Januari hadi Oktoba mwaka jana, taarifa za Benki Kuu ya Kenya (CBK) zinaonyesha Tanzania iliuza bidhaa nyingi zaidi licha ya migogoro ya kibiashara iliyojitokeza baina ya mataifa hayo makubwa.

Takwimu za CBK zinaonyesha Kenya iliagiza bidhaa zenye thamani ya Sh265.28 bilioni ndani ya muda huo ambazo ni sawa na ongezeko la asilimia 25.44 ikilinganishwa na ilivyokuwa kipindi kama hicho mwaka 2016.

Ndani ya kipindi hicho, mauzo ya bidhaa za Kenya yalipungua kwa asilimia 18.9, ikiwa ni kiwango kikubwa zaidi ndani ya muongo mmoja wa ushirikiano wa kibiashara kati ya Taifa hilo na Tanzania.

Tanzania ni muuzaji wa nne mkubwa wa bidhaa zake nchini Kenya. Takwimu zinaonyesha Afrika Kusini iliyouza bidhaa za Sh1.061 trilioni iliongoza ikifuatiwa na Misri Sh577.36 bilioni na Uganda Sh549.8 bilioni.

Kwa miezi hiyo 10 ya mwaka jana, Kenya iliagiza bidhaa za Sh3.193 trilioni kutoka Afrika ambazo ni sawa na ongezeko la asilimia 43.02 ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka uliotangulia.

Kenya inaagiza zaidi bidhaa za nguo, ngano, ngozi na kwato, mafuta ya kula, mbogamboga, mchele, karatasi, viatu, mbao, plastiki, gesi ya kupikia.