Ubadilishaji noti chakavu BoT pasua kichwa

Muktasari:

Tangu Novemba 2016, kumekuwa na matangazo ya kusitisha kutoa huduma hiyo kwa wananchi.

Dar es Salaam. Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kwa miezi miwili sasa imeendelea kusuasua kutoa huduma ya ubadilishaji wa noti chakavu na sarafu, hali inayowasababishia wananchi usumbufu.

Tangu Novemba 2016, kumekuwa na matangazo ya kusitisha kutoa huduma hiyo kwa wananchi.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti wananchi waliofika katika benki hiyo kwa lengo la kubadilisha noti na sarafu, walisema taarifa ya kurejeshwa kwa huduma hiyo imekuwa ikibadilika siku hadi siku.

“Nilipoenda kubadilisha noti mwezi uliopita nilikuta tangazo kwenye lango la kuingilia linalosema huduma ya ubadilishaji wa noti chakavu imesitishwa kwa muda na itaanza tena Novemba 28, mwaka huu,” alisema Joel Mwakasege.

Alisema siku hiyo alipokwenda alikuta tangazo hilo limebadilishwa na kuonyesha huduma hiyo ingerejea tena Desemba 5.

Huu ni usumbufu, watu wanatoka mbali lakini hawaelezwi ukweli ni lini huduma hiyo itarudishwa tena,” alilalamika Mwakasege.

Alisema juzi alikwenda na kukuta tangazo kwenye lango la kuingilia linalosema huduma hiyo itarejea Januari 2.

Akizungumzia kero hiyo, Meneja Uhusiano wa BoT, Zalia Mbeo alisema huduma ya kubadilisha noti chakavu ilisitishwa kwa muda kwa kuwa watoa huduma walitingwa na majukumu mengine.

Alisema huduma itarejea kuanzia Januari 2.

Mkazi wa Tegeta, Israel Mwinyimvua alisema tatizo siyo kusitishwa kwa huduma, bali ni matangazo ya kurejesha huduma kubadilika mara kwa mara.

“Tunawaomba siku nyingine wawe na uhakika wa matangazo wanayoyatoa kwa kuwa wanawasababishia usumbufu wananchi,” alisema.

Alisema zamani benki zilikuwa zinabadilisha noti zilizochakaa, lakini siku hizi wanazikataa na sehemu iliyobakia ni BoT.

Wananchi wengi walioshuhudiwa wakifika BoT kwa lengo la kupata huduma hiyo, walionekana kuondoka badala ya kuingia ndani kupata ufafanuzi zaidi.