Ubungo, CRDB kukopesha wajasiriamali Sh1.9 bilioni

Muktasari:

Mkurugenzi wa manispaa hiyo, John Kayombo alitoa kauli hiyo jana baada ya kusaini makubaliano na Benki ya CRDB itakayotoa huduma hiyo kwa wanawake, watu wenye ulemavu na vijana wa halmashauri hiyo.

Dar es Salaam. Manispaa ya Ubungo imesema wakati wowote itaanza kutoa mikopo yenye thamani ya Sh1.9 bilioni kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu ikiwa ni utekelezaji agizo la Serikali la kutenga asimilia 10 ya mapato ya ndani ili kuyawezesha makundi hayo.

Mkurugenzi wa manispaa hiyo, John Kayombo alitoa kauli hiyo jana baada ya kusaini makubaliano na Benki ya CRDB itakayotoa huduma hiyo kwa wanawake, watu wenye ulemavu na vijana wa halmashauri hiyo.

Kayombo alisema mikopo hiyo itatolewa makundi hayo ya manispaa hiyo yenye kata 14 kwa njia ya vikundi vya ujasiriamali.

“Ni fursa kwa vijana na wanawake watakaobahatika kupata mikopo hii. Sitarajii kuchukua mikopo hii kufanya shughuli tofauti na malengo waliyojipangia,” alisema Kayombo.

Alisema licha ya wanawake na vijana, mikopo hiyo itawahusu watu wenye walemavu waliotengewa asimilia 20 ya fedha hizo ili kuinua kipato chao na kujikwamua na umaskini.

Akizungumza kwenye hafla hiyo, meya wa Manispaa ya Ubungo, Boniface Jacob alisema walishindanisha benki nyingi, lakini CRDB iliibuka kidedea baada ya kukidhi vigezo kikiwamo cha riba ya asilimia nane ya mkopo.

“Hii ni furaha ya pekee kwa manispaa hii, kwa sababu ina mwaka mmoja na nusu tangu kuanzishwa.Lakini tumehakikisha agizo la Serikali linatekelezwa kwa ufanisi tena kwa kiwango kikubwa cha fedha,” alisema Jacob.

Jacob alisema baadhi ya changamoto ikiwamo kuchelewesha mikopo kwa waombaji zilizokuwa zikijitokeza wakati akiwa Manispaa ya Kinondoni, zimeshughulikiwa na wahusika watapata fedha zao ndani ya siku saba hadi 14 baada kuomba. Alisema hadi sasa zaidi ya wanawake 11,000 kupitia vikundi vyao wamesajiliwa kwa ajili kupata mikopo na kwamba, tayari wamepewa vigezo wakati vijana ni 1,240 nao wamesajiliwa.

Pia, Jacob ambaye pia ni diwani wa Ubungo, aliwataka wanawake, vijana na walemavu kuchangamkia fursa hiyo kwa sababu manispaa hiyo imefanya kazi kubwa ya kukusanya fedha hizo kwa ajili ya kuwawezesha.

Naye mkurugenzi wa huduma za benki mbadala wa CRDB, Philip Alfred alisema mikopo hiyo itatolewa kwa kuzingatia vigezo vilivyowekwa na manispaa ili kuwezesha makundi hayo kujikwamua na umaskini. “Ni matarajio yangu kuwaona wanawake, vijana na walemavu wa Ubungo wakipiga hatua ya maendeleo baada ya kupata mikopo hii. Mikopo hii itarudishwa kwa wakati ili mchakato huu uwe endelevu,” alisema Alfred.

Ofia maendeleo ya jamii wa manispaa hiyo, Mercy Ndekeno alisema kiwango cha mikopo kitanzia Sh300,000 na kuendelea kwa wanawake, vijana na walemavu kupitia vikundi vyao vilivyosajaliwa.

Ndekeno alitaja baadhi ya vigezo vinavyotakiwa kupata mikopo hiyo ni vikundi kutambuliwa na manispaa hiyo, kuwa na akaunti na shughuli watakayoifanya baada ya kupata mkopo huo.