Ujenzi kiwanda cha mihogo Handeni waiva

Muktasari:

Kiwanda hicho kitakachotumika kusindika mihogo, kinatarajia kuwahakikishia soko la uhakika wakulima baada ya mwekezaji kutoka nchini humo kuanza utaratibu wa kukijenga.

Handeni. Baada ya kutembelea maeneo mbalimbali nchini ili kuona namna wanavyoweza kukidhi mahitaji, Wachina wameamua kuanzisha kiwanda eneo la Kwamsisi wilayani hapa.

Kiwanda hicho kitakachotumika kusindika mihogo, kinatarajia kuwahakikishia soko la uhakika wakulima baada ya mwekezaji kutoka nchini humo kuanza utaratibu wa kukijenga.

Kiwanda hicho kitakachogharimu Dola 10 milioni za Marekani (zaidi ya Sh22 bilioni) kitaanza Septemba. Mwekezaji huyo anahitaji zaidi ya tani milioni moja za mihogo kwa mwaka. Mwakilishi wa mwekezaji huyo kutoka China, Zhang Qiang aliyetembelea eneo kitakapojengwa kiwanda hicho, alisema mihogo ya Tanzania ni bora, ndio maana wamelazimika kufanya uwekezaji huo.

Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Godwin Gondwe alisema utaratibu wa kujenga kiwanda hicho kuanzia ofisi ya mkuu wa mkoa mpaka kijijini hapo umekamilika na kilichobaki ni utekelezaji. Zaidi ya wananchi 200 wa kata hiyo na maeneo ya jirani wataajiriwa.