Vicoba kutoa mikopo ya nyumba

Muktasari:

  • Mwenyekiti wa Viguta Taifa, Dk Dauda Salmin alisema hayo jana na alipozungumza na madiwani na watumishi wa Halmashauri ya Moshi akiwahamasisha kujiunga na mkopo huo nafuu.

Muungano wa Vicoba Tanzania (Viguta) unatarajia kutoa mikopo ya nyumba 1,800 za gharama nafuu kwa wanachama wake na wajasiriamali wadogo mkoani Kilimanjaro.

Mwenyekiti wa Viguta Taifa, Dk Dauda Salmin alisema hayo jana na alipozungumza na madiwani na watumishi wa Halmashauri ya Moshi akiwahamasisha kujiunga na mkopo huo nafuu.

“Tumekuja kuangalia namna ya kuwasaidia wajasiriamali wadogo. Tunajua, kupitia madiwani ni rahisi kuwafikia,” alisema Dk Salmin.

Mwenyekiti huyo alibainisha alisema Sh900 milioni zimetengwa kufanikisha hilo na utekelezaji umepangwa kuwa ndani ya kwa miezi mitano ijayo.

Muungano huo wenye matawi nchi nzima una wanachama milioni 7,268 ambao Viguta inasema wengi wana kipato cha chini na matumizi yao kwa siku hayazidi Sh5,000 hivyo wamebuni mpango utakaowawezesha kumiliki nyumba.

Nyumba zinazotarajiwa kujengwa ni za kati ya Sh5 milioni hadi Sh25 milioni ili kila mmoja aweze kumudu gharama hizo.

Diwani wa TPC, Rogers Mmari alisema: “Nyumba ya Sh5 milioni kuilipa kwa awamu ni nafuu sana. Ni jambo zuri kwa maisha ya kila Mtanzania.”