Wafanyabiashara Wajerumani wafungua ofisi ya uwekezaji

Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Geofrey Mwambe

Muktasari:

  • Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Geofrey Mwambe alisema hilo jana katika kikao kati ya kituo hicho na wafanyabiashara hao.

Umoja wa wafanyabiashara wa Ujerumani umefungua ofisi nchini kuratibu uwekezaji wa wanachama wake na kurahisisha mawasiliano kati yao na wazawa.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Geofrey Mwambe alisema hilo jana katika kikao kati ya kituo hicho na wafanyabiashara hao.

Alisema umoja huo umeambatana na mjumbe wa kamati ya Bunge la Ujerumani anayeshughulikia uchumi na biashara na maofisa wawili wa Serikali kutoka wizara ya maendeleo ya kiuchumi.

“Wafanyabiashara hawa wamefikia hatua hii baada ya kuridhishwa na mazingira mazuri ya uwekezaji Tanzania. Ofisi kama hii ipo Nairobi (Kenya) lakini kutokana na umuhimu uliopo wameamua kufungua Tanzania pia,” alisema.

“Wafanyabiashara wa Tanzania hasa wanachama wa Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF) na wajasiriamali wahakikishe wanatumia fursa za uwekezaji utakaofanywa na Wajerumani ili kuinuka kibiashara kwa sababu wanapenda kuwa na ushirikiano na kampuni za wazawa,” alisema Mwambe.

Mkuu wa ofisi hiyo, Dk Jennifer Shcwarz alisema watahakikisha wanarahisisha biashara na kampuni za Kijerumani zitakazoonyesha nia ya kuwekeza nchini, ofisi hiyo itakuwa msaada mkubwa kwao.