Wafanyabiashara wakaidi kufungiwa maduka ya dawa

Muktasari:

Serikali yaombwa kutoa elimu kwa wananchi ili watambue dalili za Kifua Kikuu

Waziri wa Afya Zanzibar, Hamad Rashid Mohammed ametoa onyo kwa wafanyabiashara watakaogundulika kuuza dawa zinazotolewa na Serikali bure kwamba watanyang’anywa leseni na kufungiwa biashara zao.

Alitoa onyo hilo katika kilele cha maadhimisho ya Siku ya Kifua Kikuu (TB) Mjini Unguja juzi na kuongeza kuwa hatua hiyo ni moja kati ya juhudi za kusimamia upatikanaji wa huduma za afya kwa kiwango kinachotakiwa.

Alisema licha ya Serikali kutumia zaidi ya Sh10 bilioni kununua dawa na kuzitoa bure kwa wagonjwa, imegundulika kuwa wapo wafanyabiashara wanaoziuza.

Mohammed alitaja baadhi ya dawa zilizobainika kuuzwa kuwa ni za Malaria na uzazi wa mpango.

“Mfanyabiashara ambaye tutambaini kuhusika na uuzaji wa dawa ambazo sisi hutoa bure kwa wananchi wetu, ajiandae kufungiwa leseni ya kufanya biashara hata awe anauza kidonge kimoja tu cha dawa adhabu hiyo itamkumba tu,” alisema Mohammed.

Akizungumza kuhusu Kifua Kikuu, alisema Serikali imedhamiria kupambana na ugonjwa huo ambao unaonekana kuathiri jamii.

Pia, alisema Zanzibar imefanikiwa katika mapambano dhidi ya Malaria na kwamba ipo haja ya kuelekeza nguvu kwenye magonjwa.

“Kila kiongozi akiwajibika ipasavyo hakuna uwezekano wa Kifua Kikuu kushambulia wananchi wetu kama ilivyo sasa,” alisema Mohammed.

Mwakilishi wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Dk Andemichel Ghirmay aliiomba Serikali kuongeza juhudi za kutoa elimu kwa wananchi ikiwamo kutambua dalili za Kifua Kikuu na namna ya kujikinga.

Alisema WHO inajivunia kufanya kazi na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) kutokana na ushirikiano wanaoutoa kwa shirika hilo.

Meneja wa Kitengo Shirikishi cha Ukimwi, Kifua Kikuu na Ukoma, Farhat Khalid aliiomba Serikali na wananchi kuufanya ugonjwa wa Kifua Kikuu kuwa ajenda ya kudumu katika vikao vyao.