Wafugaji walalamika kukosa soko la maziwa

Muktasari:

  • Takwimu za Bodi ya Maziwa Tanzania zinaonyesha unywaji wa maziwa nchini ni wastani wa lita 47 kwa mtu mmoja kwa mwaka

 Wafugaji wa ng’ombe wa maziwa wilayani Kinondoni wamelalamikia maziwa kukosa soko hali inayosababisha wayamwage.

Walitoa kilio hicho mbele ya Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Ally Hapi wakati wa uzinduzi wa Mtando wa Wafugaji wa Ng’ombe wa Maziwa.

Katibu wa mtandao huo, Faustine Mbassa alisema kuna changamoto ya kuwapata wateja wanaohitaji maziwa.

“Kuna wakati huwa tunamwaga maziwa kwa kukosa soko, lakini maeneo mengine wanatafuta maziwa na hawayapati,” alisema Mbassa.

Alifafanua kuwa wameamua kuanzisha mtandao huo ili wawe na umoja wa kutafuta masoko ya maziwa.

Hata hivyo, Takwimu za Bodi ya Maziwa Tanzania (TDB) zinaonyesha kuwa unywaji wa maziwa nchini ni wastani wa lita 47 kwa mtu mmoja kwa mwaka wakati Shirika la Chakula Duniani (Fao) linapendekeza kunywa lita 200.

Nchini Kenya, unywaji wa maziwa ni wastani wa lita 120 kwa mtu mmoja kwa mwaka wakati Uganda ni lita 50 kwa mtu mmoja.

Akifafanua, Mbassa alisema pamoja na kwamba uzalishaji wa maziwa kwa Tanzania uko chini ukilinganisha na nchi za Afrika Mashariki lakini yanakosa soko.

Mwenyekiti wa mtandao huo, Joakim Lyaupe alimwomba mkuu wa wilaya kuwapatia maeneo ya wazi ambayo watayatumia kwa ajili ya kuuzia maziwa.

“Tunaomba Serikali itupatie maeneo ya wazi ili tuyatumie kuuzia maziwa, kwa kufanya hivyo wananchi watafahamu wapi wanaweza kupata maziwa,” alisema Lyaupe.

Aliomba Serikali kuongeza idadi ya maofisa ugani ili waweze kutoa elimu kwa wafugaji.

Kwa mujibu wa taarifa za mtandao huo, kuna vikundi 13 vya wafugaji wenye jumla ya wanachama 261.