Wajichimbia kuondoa vikwazo vya biashara

Muktasari:

  • Ufanyaji wa biashara ndani ya Bara la Afrika unaathiriwa na vikwazo vya kibiashara.

Wadau kutoka nchi za Afrika wanakutana jijini hapa kwa siku tatu kujadili namna ya kuondoa vikwazo vya kibiashara.

Pia, watajadili kuanzisha mfumo utakaotatua changamoto za kufahamu usalama wa masoko katika nchi hizo.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda,  Biashara na Uwekezaji, Profesa Adolf Mkenda amesema changamoto inayolikabili Bara la Afrika katika biashara ni kuwepo kwa utitiri wa vikwazo kibiashara.

Amesema warsha hiyo imewakutanisha wadau kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Jumuia ya Uchumi ya Nchi za Afrika Magharibi (Ecowas),  Jumuia ya Afrika Mashariki (EAC) na taasisi za kibiashara katika Bara la Afrika kujadili namna ya kuondoa changamoto hizo.

Amesema mkutano huo pia utajadili namna ya kujenga mifumo ya kuongeza taarifa za kibiashara na upatikanaji wa fedha katika nchi za Afrika.

“Kama mtu anataka kuuza bidhaa anatakiwa kufahamu viwango, malipo, usalama, kuhakikisha taarifa zinakusanywa na Bara zima la Afrika kujenga mfumo ili ziweze kutumika na wafanyabiashara wote,” amesema.

Profesa Mkenda amesema changamoto ya ufanyaji biashara inajionyesha wazi katika Bara la Afrika, kwa kuwa licha ya kuwa la pili kwa wingi wa watu na kuwa na rasilimali za kutosha, mchango wake katika biashara duniani hauzidi asilimia tatu.

Amesema “Kwa kiwango hiki hata uzalishaji utapungua, hivyo kuna mambo ya kujadili kwa pamoja ili kuongeza uzalishaji. ”

Profesa Mkenda amesema ufanyaji biashara ndani ya Bara la Afrika ni asilimia 14, kulinganisha na ilivyo Ulaya ambayo ni asilimia 70.

Mkuu wa kitengo cha biashara cha Umoja wa Afrika, Nadir Merah amesema mkutano huo utatumika kujadili namna ya kuondoa vikwazo vya kiuchumi katika nchi za Afrika.

Pia, watajadili namna ya kupata fedha za kufanya biashara na miundo ya upatikanaji wa taarifa.

“Kama kuna mtu anataka kuuza bidhaa Ivory Coast anatakiwa kupata taarifa namna anavyoweza kuingia katika soko la nchi hiyo, viwango vya fedha vikoje na hata akitaka kuwekeza katika nchi hiyo afahamu akiwa nchini mwake, badala ya kulazimika kwenda huko,” amesema.

Amesema mfumo wa taarifa ukiwepo utarahisisha kupanua uzalishaji wa ndani wa kila nchi.