Wakulima 2,000 kukilisha kiwanda kipta cha alizeti

Muktasari:

Akizungumza kwenye uzinduzi wa jengo la kiwanda cha kukamua mafuta ya alizeti mwishoni mwa wiki iliyopita juzi, meneja mkuu wa ushirika wa Ibuka Multipurpose Co-operative Society Ltd, Musiba Mkama alisema kutokana na ugawaji mbegu hizo wanatarajia uzalishaji kuongezeka.

       Kahama. Baada ya kutegemea pamba kama zao la biashara kwa miaka mingin, wakulima 2,000 wilayani hapa wamepatiwa mbegu za alizeti ili kuongeza mazao ya biashara yaliyokuwapo kukumbwa na magonjwa katika uzalishaji wake.

Akizungumza kwenye uzinduzi wa jengo la kiwanda cha kukamua mafuta ya alizeti mwishoni mwa wiki iliyopita juzi, meneja mkuu wa ushirika wa Ibuka Multipurpose Co-operative Society Ltd, Musiba Mkama alisema kutokana na ugawaji mbegu hizo wanatarajia uzalishaji kuongezeka.

“Wakulima 2,000 kila mmoja amepewa kilo mbili za alizeti, lengo ni kuwapatia wanachama wote 4,772,” alisema.

Kufunguliwa kwa kiwanda hicho kinafanya idadi ya viwanda vinavyosindika mafuta wilayani Kahama kufikia viwili.

Hata hivyo, Singida moja ya mikoa inayotegemea zaidi usindikaji wa mafuta ya alizeti una viwanda 120, vikubwa ambavyo hutegemea malighafi inayozalishwa ndani ya mkoa na mikoa jirani.

Viwanda hivyo vina uwezo wa kusindika tani 434,725 za alizeti kwa mwaka, wakati hali halisi ya upatikanaji malighafi ni wastani tani 160,000 kwa mwaka hivyo kuwapo upunfufu wa tani 274,725.

Mkama alisema uwezeshaji wa wanachama wa ushirika huo ni moja ya mikakati ya kupata malighafi itakayotumika kwenye kiwanda hicho chenye uwezo wa kusindika tani nne za alizeti.

Awali, mwenyekiti wa ushirika huo, Raphael Buhulula alisema licha ya kuwanunulia mbegu wakulima hao, wametenga eka 500 kwa ajili ya kilimo hicho ili kuendelea kukiwezesha kiwanda kufanya kazi.

Buhulula alisema mwaka jana walilima eka 35 lakini kutokana na hali mbaya ya hewa walivuna magunia 208, ambayo yatakuwa ya kianzio kwa kiwanda hicho ambacho mpaka kukamilika kitagharimu zaidi ya Sh90 milioni.

Naye mrajisi msaidizi wa vyama vya ushirika mkoani Shinyanga, Shose Monyo aliwataka viongozi hao kuwa makini ili wasiingize wanasiasa kwenye ushirika, kwani hali hiyo inaweza kuwakwamisha.

Shose alisema kwa mkoa wa Shinyanga, Ibuka ni ushirika ulionyesha mafanikio makubwa kwa kujiendeleza ikiwamo uanzishwaji kiwanda hicho, kumiliki ardhi wanaoitumia kwa kilimo na kuwa na vitendea kazi matrekta matatu.