Wasaini mkataba kunufaika na bomba la mafuta

Muktasari:

Mkataba umesainiwa kati ya umoja wa watoa huduma za mafuta na gesi Tanzania na Uganda ili kunufaika na fursa za mradi.

Umoja wa watoa huduma za mafuta na gesi nchini (Atogs) umesaini mkataba wa makubaliano na wenzao wa Uganda ili kunufaika na fursa zilizopo katika mradi wa ujenzi wa bomba la mafuta la kutoka Hoima hadi Tanga.

Mkataba huo umesainiwa leo Jumatano siku moja baada ya mkutano wa kimataifa wa wadau wa mafuta na gesi uliofanyika jijini hapa.

Makamu Mwenyekiti wa Atogs, Abdulsamad Abdulrahim amesema mkataba huo utasaidia wawekezaji wazawa katika nchi hizi mbili kunufaika na fursa zitakazojitokeza.

Mwenyekiti wa umoja huo nchini Uganda (Auogs), Emmanuel Mugarura amesema maandalizi yalianza tangu mwaka 2012 lakini wana jukumu la kutoa uzoefu wao kwa nchi rafiki ambazo zimechelewa katika maandalizi.

"Kampuni zilizopo katika nchi zetu bado hazijawa na uwezo wa kuhudumu katika mradi mkubwa kama huu lakini zikiungana zinaweza," amesema Mugarura.

Amesema endapo kampuni hizo zitashirikiana zitaweza kutoa huduma kwa haraka.

Mugarura ametoa mfano wa usafirishaji wa vifaa, akisema kampuni ya Tanzania inaweza ikavipokea bandarini na kuvipeleka mpakani mwa Uganda na baadaye kampuni ya Uganda ikamalizia safari.