Wazalishaji nondo waomba zitokazo nje zidhibitiwe

Muktasari:

  • Mwenyekiti wa Wamiliki wa Viwanda vya Chuma, Lawrence Manyama alisema hayo kwenye mkutano wao na Tume ya Ushindani (FCC) ukiwa ni mwendelezo wa kuwajengea uwezo wazalishaji na wafanyabiashara kupambana na bidhaa bandia.

Wazalishaji wa bidhaa za chuma nchini wameiomba Serikali kudhibiti nondo zisizokidhi viwango na ubora kutoka nje ili kulinda viwanda vya ndani.

Mwenyekiti wa Wamiliki wa Viwanda vya Chuma, Lawrence Manyama alisema hayo kwenye mkutano wao na Tume ya Ushindani (FCC) ukiwa ni mwendelezo wa kuwajengea uwezo wazalishaji na wafanyabiashara kupambana na bidhaa bandia.

Alisema ingawa Tanzania haizalishi asilimia 100 ya nondo zinazohitajika nchini, lakini viwanda vyake vinapaswa kulindwa.

Takwimu za Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji zinaonyesha uzalishaji wa nondo ni tani 600,000 za ujazo ingawa mahitaji ni tani 700,000.

Akijibu hoja hizo, naibu katibu mkuu wa wizara hiyo anayeshughulikia viwanda, Ludovick Nduhiye aliahidi kulifanyia kazi suala hilo.

Mkurugenzi mtendaji wa FCC, John Mduma alisema wanaendelea kutoa elimu kwa wananchi ili kuzitambua bidhaa bandia na kufikisha malalamiko yao sehemu husika ili wapate haki wanayostahili.