Wafunga lango la Mlima Kilimanjaro

Mlima Kilimanjaro

Muktasari:

“Hapa nilipo nakimbia kuelekea Marangu mtoni, polisi wanapiga mabomu wameshapiga mabomu kama matano lakini wananchi nao wanakimbia huku wakifunga barabara kwa mawe,alisema Mlay.

POLISI wa Kutuliza Ghasia (FFU) jana, walilazimika kufyatua mabomu ya machozi kuwatawanya wananchi waliofunga lango kuu la Hifadhi ya Mlima Kilimanjaro (Kinapa).

Vurugu katika lango hilo lililopo Marangu ,Wilaya ya Moshi Vijijini zilianza saa 5:00 asubuhi kutokana na wananchi hao kuandamana kupinga kile walichodai askari wawili kumbaka mwanamke mmoja.

Inadaiwa kuwa juzi asubuhi, askari wawili wa Kinapa walimbaka mwanamke mmoja (jina limehifadhiwa) ambaye aliingia ndani ya eneo la hifadhi kwa ajili ya kuokota kuni.

Habari hizo zilidai kuwa, hali ya mwanamke huyo ni mbaya kutokana na wabakaji hao kumpasua sehemu za siri na kusababisha kushonwa nyuzi kadhaa ili kuokoa maisha yake.
Mwanamke huyo inadaiwa bado amelazwa katika Hospitali ya Kilema na kuna taarifa zilizozagaa kuwa kutokana na unyama aliofanyiwa, kizazi kiliharibika na mimba kutoka.

Habari zilizopatikana kutoka eneo la tukio zilidai kuwa wananchi kati ya 200 na 300 wakiwa na mawe makubwa walifunga barabara hiyo kwa saa tano kabla ya polisi wa FFU kuamua kutumia nguvu.

Vurugu hizo zilisababishwa watalii waliokuwa wameshuka Mlima Kilimanjaro na wale waliokuwa  wakielekea katika lango hilo kupanda mlima, kukwama hadi polisi walipotumia mabomu ya machozi.

Mmoja wa mashuhuda , Jullius Mlay alidai polisi walianza kurusha mabomu hayo ya machozi saa 8:30 mchana baada ya jitihada za kuwataka wananchi hao kutawanyika kwa amani kushindikana.

“Hapa nilipo nakimbia kuelekea Marangu mtoni, polisi wanapiga mabomu wameshapiga mabomu kama matano lakini wananchi nao wanakimbia huku wakifunga barabara kwa mawe,alisema Mlay.
Wananchi hao waliandamana kwa lengo la kushinikiza uongozi wa Kinapa kuwatoa askari wake wanaotuhumiwa kushiriki katika tendo hilo la ubakaji wa mwanamke huyo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro,Robert Boaz alithibitisha kuwapo kwa taarifa za tukio la ubakaji na kwamba linadaiwa kutokea juzi katika eneo la Mbahe ndani ya hifadhi ya mlima huo.

“Kwanza huyo mwanamke hakufungua kesi, lakini kilichopo ni kwamba baada ya kufanyiwa kitendo hicho na kurudi nyumbani ndugu zake walimpeleka hospitali ya Kilema kwa matibabu,”alisema.

Kwa mujibu wa Kamanda Boaz, juzi jioni alijitokeza mwanamme mmoja aliyedai ni ndugu wa mwanamke huyo na kuripoti tukio hilo la ubakaji katika kituo cha Polisi mji mdogo wa Himo

“Hili ni tatizo la kihalifu na mpaka sasa hatujui ni nani walihusika kama ni askari wa Kinapa ama ni watu wengine ambao nao waliingia ndani ya hifadhi…tunaendelea kuwatafuta,”alisema.
Kamanda Boaz alisema polisi wanaendelea na taratibu za kiupelelezi ili kuwabaini waliohusika na kuwataka wananchi kuwa watulivu wakati polisi wakilichunguza tukio hilo kwa uzito wake.