Kiwanda chaagiza asali nje ya nchi

Asali

Muktasari:

Liu alisema hali hiyo inatokana na kukosa asali bora ya kutosha kutoka kwa wafugaji nchini.Alisema kuna mikoa mingi yenye asali, lakini wanapoichukua nyingi haina ubora

Pwani. Uongozi wa Kiwanda cha Kuchakata Asali cha Honey King, wilayani Kibaha, mkoani Pwani, umeomba Serikali kupitia Kamati ya Bunge ya Viwanda na Biashara, kuhakikisha wafugaji wa nyuki wanajengewa uwezo ili kuzalisha asali bora.

Hatua hiyo itakiwezesha kiwanda hicho kupata asali ya kutosha tofauti na sasa.
Akizungumza baada ya kamati hiyo kukagua kiwanda hicho,  Mkurugenzi Mkuu, Jack Liu alisema kiwanda hicho tangu kilipozinduliwa Juni mwaka jana na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda  hakijatimiza lengo lake la kuzalisha tani 10,000  za asali kwa mwaka.

Liu alisema hali hiyo inatokana na kukosa asali bora ya kutosha kutoka kwa wafugaji nchini.
Alisema kuna mikoa mingi yenye asali, lakini wanapoichukua nyingi haina ubora, kwani baadhi ya wakulima huchanganya sukari guru, hivyo kulazimika kuagiza kiasi kidogo kutoka nchi jirani ili wasisimamishe uzalishaji.

Aliongeza kuwa anaamini iwapo Serikali itawajengea uwezo wafugaji nyuki kwa kuwapa mafunzo au  wataalamu kutembelea mashamba yao mara kwa mara  upo uwezekanao wa kupatika asali ya kutosha.

“Hatujazalisha kama tulivyolenga wakati ule alipofika Waziri Mkuu hapa, maana tulilenga kuzalisha tani 10,000 kwa mwaka, lakini kumbe huko tulikotegemea kupata asali kuna changamoto kubwa kwelikweli,” alisema Liu na kuongeza: “Naomba Serikali kutilia mkazo uzalishaji wa kutosha wa asali, ili  tukidhi mahitaji ya kiwanda ya kuzalisha tani 10,000.”

Awali, Mkuu wa Mkoa wa Pwani,  Mwantumu Mahiza alitoa taarifa ya hali ya mkoa huku aliweka wazi kuwa kiwanda hicho tangu kuzinduliwa Juni mwaka jana hakijafanya uzalishaji wowote.