Intaneti zafungwa Congo Brazzaville

Muktasari:

Wiki iliyopita Serikali ilitangaza kuyapiga marufuku maandamano yaliyoitishwa na wapinzani waliokuwa wakimpinga Rais Nguesso kutaka kuendelea kukaa madarakani kwa awamu ya tatu.

Brazzaville, Kongo. Serikali ya Congo Brazzaville imesitisha huduma za mtandao na kufunga mawimbi ya redio ya Kimataifa ya Ufaransa (RFI) nchini humo.

Pia, Serikali imetangaza kusimamisha huduma nyingine za mawasiliano ikiwamo ujumbe mfupi wa simu katika hatua zake za kukabiliana na wimbi la maandamano yanayoratibiwa na wapinzani.

Hatua hizo zimechukuliwa ikiwamo imepita siku moja, baada ya watu wanne kuuawa mjini Brazzaville katika makabiliano baina ya vikosi vya usalama na wafuasi wa upinzani wanaopinga kura ya maoni kuhusu katiba mpya.

Wapinzani wamekuwa wakiandamana kupinga vikali kura ya maoni ya katiba mpya ambayo inampa Rais Dennis Sassou Nguesso uwezo wa kugombea urais nchini humo katika uchaguzi mkuu ulipangwa kufanyika baadaye mwaka 2016.

Kwa mujibu wa katiba ya sasa, Rais Sassou Nguesso mwenye umri wa miaka 72 hawezi kugombea urais kwa mara nyingine.

Katiba inaeleza kwamba hawezi kugombea urais kwa sababu amemaliza mihula yake miwili.

Hata hivyo, katika katiba mpya iliyopendekezwa vizingiti hivyo viwili vimeondolewa na hivyo kumfungulia njia kiongozi huyo wa siku nyingi kugombea tena nafasi ya urais ili kurudi madarakani.

Rais Nguesso alikuwa rais tangu mwaka 1979 hadi 1992.

Baadaye alikuwa kiongozi wa upinzani na kurejea madarakani baada ya vita vya ndani nchini humo mwaka 1997 vilivyogharimu maisha ya raia wadhaa.

Wiki iliyopita Serikali ilitangaza kuyapiga marufuku maandamano yaliyoitishwa na wapinzani waliokuwa wakimpinga Rais Nguesso kutaka kuendelea kukaa madarakani kwa awamu ya tatu.

Wapinzani hao wanataka kuheshimiwa kwa katiba iliyopo na wametishia kuendelea na maandamano iwapo jaribio hilo la kurekebisha katiba halitasitishwa na serikali iliyopo madarakani.

Hivi karibuni wakati akiwa nchini Ethiopia, Rais Barack Obama wa Marekani aliwaonya baadhi ya viongozi wa Afrika wanaopenda kubadili katiba ili waendelea kusalia madarakani.

Alisema kuwa hali kama hiyo siyo tu inakwamisha ukuaji wa demokrasia lakini pia inarudisha nyuma maendeleo ya wananchi.

Kwa hivi sasa kumekuwa na vuguvugu linaloendelea katika baadhi ya nchi kutaka kubalisha katiba ili viongozi walioko madarakani waendelee kusalia madarakani.

Tayari nchini Rwanda bunge limepitisha muswaada unaotaka kuitishwa kwa kura ya maoni ili kumwezesha Rais Paul Kagame kuwania muhula mwingine.

Pia, kumekuwa na vuguvu lingine katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo kutaka kurekebisha sehemu ya vipengele vya katiba ili kutoa nafasi kwa Rais Joseph Kabila kuwania muhula mwingine wa uongozi. Wapinzani wamekuwa wakikosoa vikali hali hiyo.