‘Mpishi wa filamu za Bongo Movie aliyeweka kapuni’ shahada ya uhandisi

Mtunzi na mwongozaji wa filamu maarufu za Bongo Movie, Daniel Leonard Manege.

Muktasari:

Manege ambaye ameandika filamu nyingi maarufu zinazosisimua watazamaji nchini, alisema kuwa atatumia taaluma na uzoefu alionao wa miaka minne sokoni kuhakikisha anaziba mianya yote ya uharibifu dhidi ya kazi yake.

Dar es Salaam. Mtunzi na mwongozaji wa filamu maarufu za Bongo Movie, Daniel Leonard Manege ametangaza kuachia filamu mpya akilezeza kuwa atatumia mfumo tofauti wa masoko ili kuhakikisha filamu hiyo iitwayo “Safari ya Gwalu” inawafikia wananchi katika ubora unaotakiwa.

Manege ambaye ameandika filamu nyingi maarufu zinazosisimua watazamaji nchini, alisema kuwa atatumia taaluma na uzoefu alionao wa miaka minne sokoni kuhakikisha anaziba mianya yote ya uharibifu dhidi ya kazi yake.

Mwongozaji huyo aliyehitimu Shahada ya Uhandisi wa Viwanda na Utawala kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), alisema ametumia zaidi ya Sh20 milioni kutayarisha filamu hiyo mpya ambayo mwigizaji mkuu ni Gabo Zigamba na kwamba inamzungumzia kijana aliyekwama kimaisha ambaye aliamua kurudi shule ya msingi ili apate elimu.

“Nimeshaandika filamu nyingi zilizofanya vizuri sokoni na kujitwalia tuzo nyingi za filamu hasa kwenye tamasha la Ziff kila mwaka. Lakini Safari ya Gwalu’ ni filamu yangu ya kwanza kuiandaa. Niliamua kumtumia Gabo kwenye filamu hii kwa sababu alifanya vizuri katika Filamu ya Bado Natafuta. Hiyo pia niliiandika mimi. Kwa mujibu wa muswada wa Filamu ya Safari ya Gwalu, niliona Gabo anafaa na amefanya ilivyotakiwa.” alisema Manege.

Alisema mapenzi yake katika tasnia hiyo yalimfanya afikirie ni namna atakavyofanya ili kuibadilisha fani hiyo, akieleza kwamba kwake hakuna hasara kuacha taaluma aliyosomea na kuingia katika uwanja wa filamu.

“Filamu yangu ya kwanza kuiandika na ikaingia sokoni na kupendwa ni; “U Me and Him”, ilikuwa chini ya Jacob Steven (JB), iliigizwa pia na JB mwenyewe, Kajala, Cloud 112,” alisema.

Alisema akiwa na JB alitunga filamu nyingi, ikiwemo; Bado Natafuta; Shkamoo Mzee; Nipende Monalisa; Dj Benny; Nakwenda kwa Mwanangu na nyinginezo.

Manage alibainisha kuwa kwa sasa ameashandika filamu zaidi 10 na zote zipo sokoni, ambapo alifanya kazi na waigizaji mbalimbali akiwamo kama Dk Cheni, Steve Nyerere, Wema Sepetu, Gabo, Shamsa Ford na wengineo.

Hata hivyo alisema licha ya kukaa kwa muda mrefu katika tasnia hiyo, hajawahi kufikiria kuwa mwigizaji bali anatamani abadili mfumo wa masoko katika tasnia hiyo.

“Nilikuwa naota ndoto za kuja kuwa mkombozi wa tasnia hii, nashukuru zimeanza kutimia kwa kuandika filamu zilizokubalika, kujenga mtandao wa masoko na hata ubora filamu zenyewe. Nilijua siwezi kuwa mwigizaji ila kuikuza tasnia.

“Unajua tasnia ya filamu imekuwa ikikosa waandishi na waongozaji, hivyo wasomi tunatakiwa kuunganisha nguvu katika sekta ya sanaa nchini kwa kuwa filamu ni sekta pekee inayoingiza kiasi kikubwa cha fedha maeneo mengi ulimwenguni pia ni muhimu sasa tusifikirie kuajiriwa muda wote,” alisema Manege.