Muziki wa Congo ulipotawala Afrika

Muktasari:

Wengine walikuwa wakipita katika baa ambazo zilikuwa na Jukebox na kusikiliza nyimbo walizokuwa wanazipenda. Jukebox ilikuwa aina ya mashine ambayo ulikuwa unaweka sarafu ya thumni (senti hamsini) au shilingi na kisha kuchagua wimbo unaoupenda na unapigwa.

Katika miaka ya 1960 na 1970 muziki na wanamuziki wa Congo walikuwa maarufu sana hapa nchini. Vijana wa wakati huo waliokuwa wanaupenda muziki wa huko walikuwa wakizisikiliza nyimbo hizo kwa makini na kuandika maneno ya nyimbo hizo katika madaftari licha ya kuwa hawakuwa wakifahamu lugha ya Kilingala na walihakikisha kila santuri mpya ya bendi ambayo walikuwa wakiipenda waliinunua.

Wengine walikuwa wakipita katika baa ambazo zilikuwa na Jukebox na kusikiliza nyimbo walizokuwa wanazipenda. Jukebox ilikuwa aina ya mashine ambayo ulikuwa unaweka sarafu ya thumni (senti hamsini) au shilingi na kisha kuchagua wimbo unaoupenda na unapigwa. Wanamuziki wengi na hata vijana wengi wapenzi wa muziki huo walijipachika majina ya wanamuziki maarufu wa enzi hizo, kuna vijana walijiita Brazos, Zozo, Bavon, Bholen, Mujos,Muzola Ngunga, Nzayad au Vata Mombasa.

Santuri za muziki huu zilikuwa zikichapishwa Kenya, hivyo ilikuwa biashara kubwa sana ya santuri hizi, na maduka na wafanya biashara wa santuri nao walipata umaarufu mkubwa katika miji waliyokuwapo kutokana na kuuza tu santuri.

Kuna mambo ambayo ukiyawaza siku hizi unajiuliza mengi, ilikuwaje vijana waliweza kujua mitindo ya uchezaji wa nyimbo mbalimbali wakati hakukuwa na runinga wala sinema za kuonyesha uchezaji huo?

Tofauti na zama hizi, wakati huo kila staili mpya ya muziki ilikuwa na aina ya uchezaji wake na kila bendi ilijitahidi kubuni namna ya kucheza muziki wake, hivyo ukiacha uchezaji wa muziki wa midundo mikubwa ya asili kama vile rhumba, chacha, bolero, na kadhalika, kulikuwa na uchezaji wa kirikiri, sukisa, pachanga, sakumuna, kavasha na mitindo mingine ya bendi za enzi hizo.

Kwa hapa Tanzania staili nyingi mpya za uchezaji zilijulikana kwanza Dar es Salaam, labda kwa kuwa kulikuwa na wanamuziki wengi wa kutoka Kongo. Nakumbuka kuwa wale wanafunzi wa shule hasa za sekondari waliokuwa wakifika Dar es salaam kwa ajili ya likizo, walihakikisha kuwa wanajifunza staili mpya zote za kucheza ili wakirudi kwenye shule zao mikoani wanakuwa ndio ‘masupasta’ kwa kuwa na staili mpya za uchezaji, na hiyo ikwa mojawapo ya njia zilizoeneza staili mpya za uchezaji.

Kutokana na kutokuwa na aina nyingi za mawasiliano, magazeti machache na redio kubwa ilikuwa moja tu, japo wengine walisikia redio za nje ya nchi, Burundi, Uganda wakiwa na redio yao ya Soroti, na wengine kusikiliza Radio toka Kinshasa, wanamuziki wengi walifahamika kwa sauti zao na vyombo walivyovipiga, sura zao ilikuwa nadra kuzifahamu, mara moja moja kulikuwa na bahati ya gazeti kutoa picha ya sura ya mwanamuziki maarufu, picha hizi zilikuwa na thamani kubwa sana.

Vijana wengi walikuwa na daftari ambazo walibandika picha za wanamuziki mbalimbali waliokuwa wakitamba, daftari hilo lilitunzwa kwa uangalifu mkubwa. Kwa wazee ambao walikuwa wapenzi wa muziki wa zamani majina kama Tabu Ley, Joseph ‘Grande Kalle’ Kasebele, Pepe Kalle,Nicholaus Kassanda maarufu kwa jina Dr Nico, Johnny Bokelo, Bavon Marie Marie, Soki Vangu na Soki Dyanzenza,Verckys, Franco na bendi zao African Jazz, African Jazz Fiesta, Conga Success, Negro Success, Kiam, Veve, Bela Bela , Lipua lipua na nyingine nyingi, majina hayo huwarudisha katika enzi ambazo wengi huamini kuwa hakutakuwa na muziki utakaoweza kufikia muziki uliopigwa katika zama hizo.

Kuna mambo yaliyotokea ambayo yanaweza kuongeza uzito imani hiyo kwani mwanamuziki kama Tabu Ley aliwahi kutunukiwa heshima katika nchi mbili nje ya nchi yake ya Kongo. Serikali ya Chad ilimpa heshima ya Officer of The National Order, wakati Senegal ilimpa heshima ya Knight of Senegal, na ndipo alipoanza kujiita Siegneur Rochereau. Hakika lazima uwe umefanya kitu kikubwa kwa nchi ambazo s ik kwenu kuamua kukupa tuzo za heshima. Hakuna anaejua kazi za Franco Luambo Luanzo Makiadi, anayeweza kubisha umuhimu wa Franco katika muziki wa Rumba barani Afrika. Franco aliyeanza muziki akiwa na umri wa miaka 12 tu alikuja kufikia kutoa album zaidi ya mia mbili ambazo zote zilionyesha umahiri wake wa kupiga gitaa kwa staili mbalimbali ambazo ziliigwa na wanamuziki wengine Afrika nzima.

Franco alifikia daraja ambalo hakuna mwanamuziki mwengine wa Afrika amefikia au anaweza kulinganishwa nae. Mdogo wake Franco, Bavon Marie Marie akiwa anapiga gitaa la solo akishirikiana na wenzie akina Leon’ Bholen’ Bombolo, Hubert ‘Djeskin’Dihunga, mpiga sax Andre Menga, mpiga gitaa la rhythm Jean Dinos, mpiga gitaa la bezi Alphonse ‘Le Brun’ Epayo, walikuwa katika bendi yao waliyoiita Negro Succes, kuanzia mwaka 1965 bendi hii nayo ilikuja kuleta msisimko Afrika nzima , na kutokana na tabia ya Bavon kujichubua, wanamuziki wengi wakaanza utamaduni huo wa kujichubua wakati huo wakitumia krim iliyoitwa AMBI.

Utamaduni wa kujichubua umekuwa sugu kuuondoka Afrika mpaka leo. Pengine methali ya Kiswahili isemayo ‘ngoma ikivuma sana hupasuka’ ndicho kilichotokea kwa muziki wa bendi wa Kongo.

Muziki unaotoka Kongo kwa sasa ni kivuli tu cha ulikuwapo enzi hiyo na hata Wakongo wenyewe katika maandiko mbalimbali wanathibitisha hilo. Na kwa wanamuziki wa Tanzania ambao wamekuwa wakijikita kuiga kila kitu kutoka Kongo nao pia wanalaumiwa kwa kuanguka kwao kwa ubora wa muziki wa dansi wa nchi hii