Nani zaidi Wema na Zari? akili zetu zimewehuka...

Muktasari:

  • Sisi bado hatujajiandaa kwa hivi vitu.

Kuna kitu kinaitwa demokrasia na kingine kinaitwa utandawazi. Hivi vitu kwa Afrika havitakiwi kuwepo. Kama kuja vingekuja baadaye sana lakini siyo kwa wakati huu. Sisi bado hatujajiandaa kwa hivi vitu.

Bado akili zetu zinatakiwa kuendeshwa kindava ndava na wababe, badala ya kuachwa tujiendeshe wenyewe kiwehuwehu tu. Hatukuwa tayari kujiendesha. Fuatilia maisha yetu kwa ngazi ya familia tu nd’o utajua sisi bado sana.

Kibaya zaidi sasa kila kitu imekuwa siasa. Maisha yamekuwa ya ovyo kuliko dhana ya maisha ilivyo kwenye akili zetu. Yaani tunatenda na kufanya vitu ambavyo havipo na havistahili kuwepo.

Sasa tazama wasomi wetu waliobobea kielimu hawataki kufundisha watoto wetu wa vyuo vikuu. Wanawaza kubishana na kuvimbiana vifua kwenye majukwaa ya siasa. Wanashupaza shingo kama vile wanakula saruji.

Wengine wameacha kusaidia taifa kujikwamua na matatizo. Wanachofanya kwa kutumia uwezo wao wa akili wanawaandikia wazungu makaratasi ya kuomba mamilioni ya pesa. Yaani vitu vyepesi vyepesi kuliko uzito wa akili yao.

Wanaenda vijijini kwa watu masikini. Wakiwa na magari kibao yenye thamani kubwa kuliko madaraja kumi au zaidi ya kuwavusha watu kwenye mito. Eti kwenda kuwauliza maskini hao kuwa nani maarufu kati ya Lowassa na Magufuli.

Umaarufu wa Lowassa au Magufuli unamsaidia nini mama yangu kijijini asiyejua utamu wa maji safi tangu taifa hili liundwe na kina Nyerere na wenzake? Eti demokrasia.

Wanapewa mabilioni ya pesa wanayatumia kwa maswali ya kibwege bwege kwa mtu ambaye hajui hata zahanati ni kitu gani. Hawa watu walitakiwa kuwa kwenye kuta nne kule Keko au Segerea. Huu ni utakatishaji wa pesa kwa gia ya demokrasia.

Na sisi watoto wa mjini tunajazana mitandaoni kama mataahira tukifurahia tunapoambiwa na hawa wasomi wahuni majizi ya wazi wazi wa mchana kweupee pee. Kuwa Lowassa ni maarufu kuliko Magufuli. So what?

Wasomi wetu hawatumii usomi wao kutusaidia kama taifa. Wao wanataka kuingiza pesa kwa ‘propozo’ za kijinga. Yaani wanapiga pesa kwa kuangalia akili zetu zinawaza nini. Kifupi ni kwamba wanatumia akili zao kubwa kuingiza pesa kwa akili zetu mbovu.

Ukiuliza faida ya hizi taasisi za utafiti utaambiwa ni demokrasia. Hii ni demokrasia au ghasia? Uhuni huu. Watu wanaingiza pesa kwa ubovu wa akili zetu. Tazama leo hii kuna vyama vya siasa vinagombea ruzuku kuliko majimbo yaliyoachwa wazi. Wanawaza pesa.

Wanasiasa wanapiga kelele majukwaani ili wapate ajira kwa mgongo wa kutetea maslahi ya Taifa. Sasa kwanini wanatumia pesa nyingi ili kupata ubunge udiwani nk? Wanajua wakiapishwa kuna pesa zaidi.

Demokrasia wakati mwingine au wakati wote ni biashara kama biashara zingine.

Angalia familia yako wanasiasa hawa nao ni sehemu ya biashara. Demokrasia imeletwa kama biashara.

Tunaambiwa dini imekuwa ni biashara. Hata demokrasia ni biashara pia. Tukitaka kusonga tuwapuuze wanasiasa na demokrasia. Hangaika na familia yako. Ila nako kwenye familia wanataka demokrasia.

Yaani watoto wanachagua nini cha kula na siyo baba wala mama. Haya maendeleo yanakuja kama mafuriko. Yanasomba kila kitu kizuri na kibaya. Na yanaleta kila kitu kizuri na kibaya.

Hivi sasa dunia ni ya utandawazi. Yaani kila kitu kiko peupe. Huwezi kumficha kitu hata mtoto. Yale mambo ya kudanganya watoto kuwa watoto wananunuliwa sokoni dunia ya sasa utaonekana chizi. Watoto wanajua ya kitoto na kikubwa.

Kwa sababu ya huu utandawazi mara nyingi tuwapo na wenzi wetu huwa tunatamani tuwe kama kina fulani tunaowaona. Yaani wasichana wanatamani kuwa kama staa fulani wa kike na wa kiume pia wana akili hizo.

Au hata tufanyapo mapenzi tumekuwa tukiingiza fikra za kuwa na mtu fulani kutoka kwenye mitandao. Lakini kubwa zaidi tumekuwa tukiiga tuyaonayo kutoka kwenye mitandaoni na kuyafanyia kazi mbele ya wenzi wetu.

Siku za hivi karibuni pamekuwapo na ongezeko kubwa la maneno kama ‘vibamia’. Hili neno limekuwa kero sana kwa wanaume wengi. Nitaongelea kidogo yaliyowahi kumkuta rafiki yangu mmoja ambaye alinisimulia.

Mshikaji wangu huyo tulifahamiana kwa njia ya mitandao tu. Aliniambia kuwa alikutana na dada mmoja ambaye alikuwa bikra. Wakati wa tendo alikuwa akilalamika sana kuhusiana na umbile lake. Eti akidai ni kubwa.

Huyo rafiki akadai kuwa alihisi pengine ni kwa sababu ya ugeni wake katika tendo. Lakini hata baada ya tendo hilo alizidi kulalamika kuwa hakuwa na umbile la kawaida. Hili lilimfikirisha sana.

Hali hii ilimfanya mshikaji amuhoji huyo binti kuwa anazungumzia umbile lake kwa kufananisha na nani? (kumbuka alikuwa bikra). Binti alikiri kuwa amekuwa akijifunza mambo haya ya mapenzi kwa kusoma katika mitandao ya kijamii.

Huko amekuwa akiona na kusikia wanawake wakilalamika juu ya udogo wa maumbile ya wapenzi wao na wengine wakienda mbali mpaka kulinganisha na kidole cha mwisho cha mkono.

Hivyo mpaka anaanza kuingia katika mapenzi amekuwa na picha yake kichwani na akili fulani kuhusu maumbile ya wanaume. Hilo tatizo wanalo wengi kupitia hii mijadala ya mitandaoni. Utandawazi huo.

Wapenzi wamekuwa na hamu/hisia za kuwa na mwanaume/mwanamke fulani kutoka kwenye mtandao. Maisha ya sasa yamekuwa rahisi sana kwa sababu ya hii mitandao. Kila kitu kipo mitandaoni.

Kwa hali hii asilimia kubwa ya ndoa nyingi hazina furaha kutokana na wanandoa kila mmoja kuhisi hakuoa/kuolewa na mtu sahihi kama ambavyo amekuwa akiona kutoka kwenye mitandao. Vijana wana wakati mgumu sasa kwa dunia ya sasa.

Lakini katika athari mbaya zaidi ya utandawazi ni pale ambapo tumekuwa tukijifunza mitindo mbalimbali kupitia mitandao. Kwa namna hii hata ukiwaita wanawake waliotelekezwa kila wiki watakuja tu. Wako wengi mno.

Nina uhakika hata wimbi kubwa la ufanyaji mapenzi kinyume na maumbile limetokana na utandawazi. Huko ndilo kwenye akili mbovu za namna hii.

Kama ilivyo dini. Mapokezi ya mitandao hii kwa Afrika imekuwa kinyume tofauti na malengo ya wenye mitandao huko duniani. Hata mauaji ya kidini mengi yako kwa kwetu kuliko kwa wenzetu waliotuletea sisi hizi imani.

Hali ni mbaya, imefika wakati wapenzi kwa kupitia wanachokiona au kusikia katika mitandao wamekuwa wakijitahidi kutafuta mwenzi wa kando (mchepuko) katika kutafuta kile wakionacho au kukisikia katika mtandao.

Imekuwa jambo la kawaida kabisa kusikia watu wakijinasibu kuwa hawawezi kufanya mtindo fulani wa mapenzi na mwenza wake. Hiyo mitindo wanafanya na michepuko. Haya ndo majanga ya utandawazi.

Athari chache za utandawazi ni kuongezeka kwa mashoga. Watoto kujua mambo mabaya. Wanaume na wanawake kuvaa nusu utupu, kujichubua, utovu wa nidhamu, kupunguza upendo, kudumaza akili nk.

Utandawazi umetengeneza matabaka mawili. Tabaka linalofaidika na utandawazi na linaloathirika na utandawazi. Sisi Waafrika asilimia kubwa ni waathirika wakubwa wa utandawazi. Kwa sababu tumekuwa watu wa mapokeo zaidi.

Kwa mfano, matumizi ya simu na kompyuta nchi ambazo hatuwezi kutengeneza tumekuwa wahanga wakubwa. Katika jambo hili la mataifa kama Marekani, nchi za Ulaya, Uchina, na Japan ni imara kiuchumi kwa sababu ya kuwekeza kwenye tekinolojia.

Utandawazi upo na vigumu kuukwepa. Cha msingi ni kuwekeza katika elimu inayotoa nguvu kazi yenye kutoa maarifa ya hali ya juu. Hili jambo litasaidia mataifa wahanga wakubwa wa utandawazi kama sisi kuanza kuwa na teknolojia zetu, na viwanda vyetu.