Wasanii wasiwe kama watoto wa majalalani

Muktasari:

  • Tafsiri ya michoro hiyo ndiyo iliyosababisha uvumbuzi wa herufi, namba, kalenda, ramani za majengo na hata madaktari waliweza kufanya upasuaji wa miili kwa kutegemea sanaa.

Iliaminika na ikathibitika kuwa mwanzo wa sanaa za duniani ni Bara la Afrika. Watafiti wa mambo ya kale walivumbua michoro kutoka Rumi, Ugiriki na Mashariki ya Mbali, lakini ile iliyotokea Misri ilionekana kuwa na umri mkubwa zaidi.

Tafsiri ya michoro hiyo ndiyo iliyosababisha uvumbuzi wa herufi, namba, kalenda, ramani za majengo na hata madaktari waliweza kufanya upasuaji wa miili kwa kutegemea sanaa.

Si michoro pekee, Waafrika walikuwa na utamaduni wa kupeana morali au tahadhari kwa kutumia sauti (nyimbo). Baadaye zilitumika ala zilizotengenezwa katika mazingira yao kama pembe za wanyama, ngoma, marimba na kadhalika. Kwa mfano, chifu alipotaka kulala alibembelezwa na zeze lakini pembe na ngoma ziliashiria wito.

Wakati wa mapinduzi ya viwanda huko Ulaya yaliathiri Afrika kwa namna nyingi sana. Kwanza ilihitajika nguvu kazi na malighafi ya kuendesha viwanda vyao. Lakini pia walivutiwa na tamaduni zetu, hivyo kundi lingine la wabunifu na wasanii lililazimishwa kwenda kuongeza morali za wachapakazi. Waliboreshewa zana zao na kuanza kutumia vinanda badala ya marimba, gitaa badala ya zeze na kadhalika.

Ni muda mrefu umepita hadi kufikia dunia isiyo na tofauti na kijiji. Ilibidi Afrika nayo kupambana na kuzalisha kile ambacho kingenunuliwa Ulaya. Kila unachokifanya huku ni lazima kiwe kimataifa kuziba pengo la manunuzi yako ya nje.

Ni bayana kuwa Mwingereza hajui Mdumange. Na ingelikuwa jambo gumu Mwafrika kuacha kupiga ngoma zake na kutarajia kuwauzia albamu za muziki wa country. Hivyo ili umuuzie Sindimba ilikupasa kuichanganya na pop au country. Hapa ndipo ulikuja umuhimu wa elimu ya alama za muziki.

Hizi kwa lugha ya kimombo zinaitwa music notation au nota. Kwa tafsiri yangu ni alama zinazoandikwa au kuchapwa kwa ajili ya kuelekeza na kutafsiri nyimbo na midundo (ala za muziki). Kwa kiasi kikubwa nota hutumiwa na makundi ya muziki wa kisomi kama kwaya na bendi za polisi.

Lakini nota zipo katika kila muziki. Tusijidanganye kwa kudhani rap ni kufoka bila utaratibu. Sikilizeni kibao cha Coolio cha See you when u get there msikie jinsi rap (rhythm na mashairi) vinavyoweza kuchanganywa na R&B (Rhythm & Blues) na kugeuka kwaya inayoweza kutumika kwenye nyumba za ibada.

Mtazame R. Kelly katika safari yake kutoka muziki mgumu (1990) hadi laini (2000). Muone jinsi anavyopanga muziki wake kwa kutumia kinanda anachopiga mwenyewe. Kamsikilize Bob Marley alivyopangilia reggae yake kwa kutumia gitaa kavu kabla hajaupeleka jukwaani au studio.

Nimepata kumsikia mpuliza ala za upepo wa Sikinde ya wakati ule akieleza jinsi alivyofundishwa muziki na mwalimu mzaliwa wa Zambia. Utaona pia ni kwa kiasi gani Wazambia kama Joseph Mulenga na Michael Enoch walichangia maendeleo chanya kwa muziki wa dansi Tanzania.

Kwa nini Wazambia?

Kama ilivyokuwa kwa jirani zake barani Afrika, Zambia ilikuwa koloni la Mwingereza.Mfumo wake wa elimu ulikuwa ‘7-5-4’; madarasa saba ya shule ya msingi, matano ya sekondari na manne ya chuo kikuu. Hata ilipojikomboa mwaka 1964, Zambia ilishikilia mfumo ulioachwa na wakoloni.

Pale mwanzoni, shule za chekechea zilifunzwa muziki japo si kwa nota. Ulipofika mwaka 2010 shule hizo zote zilibinafsishwa baada ya Serikali kujiondoa katika kuzihudumia, lakini msimamo katika masomo ya muziki ukabakia kama mwanzo ili kumuendeleza mtoto katika masuala ya jamii, uzalendo na utamaduni.

Katika elimu ya msingi somo hili liliunganishwa na ngonjera, mashairi na majigambo na kujulikana kama “sanaa elezi”. Kulikuwa na walimu waliosomea ufundishaji muziki na ilitengwa bajeti ya ununuzi wa ala. Pia kulikuwa na utaratibu wa kuwaalika wanamuziki maarufu shuleni kwa ajili ya motisha kwa watoto.

Unapofika katika elimu ya sekondari, muziki sasa unafundishwa katika mfumo wa kumjenga kijana katika maisha anayoyaingia. Anatoka hapo akiwa na uwezo kujishughulisha moja kwa moja kama mwanamuziki au kama msambazaji ama mwalimu.

Kutokana na uchumi wa Zambia kutokuwa rafiki kwa wanamuziki chipukizi, vijana wengi walikimbilia Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC). Lakini pia utawala wa DRC nao haukueleweka sawasawa, wanamuziki wengi kutoka huko walihamia Kenya na Tanzania.

Safari ya aina hii ndiyo iliyopitiwa na King Enoch ambaye awali alipiga gitaa la kuongoza la Dar Jazz na baadaye akaja Sikinde na kupuliza ala za upepo. Kadhalika yeye ndiye aliyekuwa mpangaji wa sauti zote zilizokuwa zikiimbwa na bendi (music composer/arranger).

Zaidi ya ufundi wa muziki, sifa kubwa zaidi walizonazo watu waliosomea muziki ni nidhamu. Izingatiwe kuwa dereva aliyesomea Veta anatofautiana na utingo aliyefundishwa na dereva wake. Kuna kipengele muhimu cha kujitambua ambacho dereva wa mtaani anazidiwa na yule wa chuoni.

Nadhani bado Tanzania tuna wajibu wa kukuza sanaa vyuoni iwe njia ya kurudisha uzalendo. Vijana wengi wanapita huko badala ya JKT, hivyo wataupokea uzalendo kwa hiari. Hatutasikia tena wasanii wakiimba matusi wala kucheza uchi.

Kamwe wasanii hawatafanana na watoto waliokulia majalalani.