Nkambi amtupia kijembe Muumini Mwinjuma

Muktasari:

Mpiga kinanda wa bendi ya muziki wa dansi ya The African Stars, Twanga Pepeta, Victor Nkambi amesema mwimbaji Mwinjuma Muumin ni kipepeo ambaye anataka kutua kila ua

Mpiga kinanda wa bendi ya muziki wa dansi ya The African Stars, Twanga Pepeta, Victor Nkambi amesema mwimbaji Mwinjuma Muumin ni kipepeo ambaye anataka kutua kila ua.

Akizungumza na Mwananchi kwenye viwanja vya Leaders, Nkambi alisema Muumin hana utulivu na amezoea maisha ya kuhamahama kila bendi, jambo linalochangia kushusha thamani yake.

“Muumini ni mzuri, lakini kama kipepeo anataka kutua katika kila ua, akihisi ua hili ni zuri atalirukia, akiona lingine tena atalifuata,” alisema msanii huyo na kuongeza kuwa wana amani kubwa baada ya kuondoka kwake.

“Tunajisikia amani sana kufanya kazi bila Muumini, alikuwa na mambo mengi ambayo yalitunyima amani, ni mtu mgumu sana kufanya nae kazi.

“Alikuja kwetu kusafisha nyota wacha akajaribu bahati yake sehemu nyingine, lakini ni nina uhakika hata huko akishafyonza ua na utamu ukaisha lazima atimke,” aliongeza.

Nguli huyo alikwenda mbali zaidi kwa kusema kwamba mwimbaji huyo aliyejiunga na Victoria Sound  alishindwa kuendana na mirindimo ya Twanga Pepeta.

“Muumini alishindwa kujibadilisha ili kufanana na muziki wa sasa, alisimama kwenye uimbaji wake ule ule wa tangu Mchinga Sound na hata Tamtam,” anaeleza.