Tegemeeni makubwa kwangu!

Saida Mashauzi

Mdogo  wa mwanamuziki wa miondoko ya taarabu  nchini, Isha Ramadhani Mashauzi,Saida Mashauzi,amesema kuwa nia yake siyo kuimba nyimbo za kunakili bali kuwa na nyimbo zake mwenyewe.

Saida alisema hayo kufuatia kuimba nyimbo za dada yake kwa ustadi mkubwa na kama hukumwona anavyoimba huwezi kusikia tofauti.
Alisema kuwa lengo lake ni kuwa msanii wa kimataifa kama dada yake na kuwa na mafanikio makubwa na uwezo anao hivyo mashabiki wake wakae mkao wa kula.

"Uwezo wa kufanya maajabu kwenye muziki ninao naimba nyimbo za Isha kwa kuwa bado najipanga kwani hata wanamuziki wakali duniani walianza kwa kuimba nyimbo za wasanii wenzao ili kujipanga kuwa na za kwao,na ninazo zangu ambazo zitatoka muda si mrefu", alisema Saida.

Saida ambaye ni mwanamuziki kwenye bendi ya dada yake ya Mashauzi Clasic, aliongeza kuwa ana matumaini makubwa kuwa bendi hiyo itazidi kufanya vizuri kutokana na kuwa na wasanii wakali na wenye uchu wa maendeleo.