Kajala Masanja na huruma ya Wema Sepetu

Muktasari:

Muigizaji Wema Sepetu, amesema kuwa alilazimika kumsaidia msanii mwenzake Kajala Masanja kwa kujua ipo siku na yeye atakuwa na tatizo na atahitaji msaada kutoka kwa wengine.

Muigizaji Wema Sepetu, amesema kuwa alilazimika kumsaidia msanii mwenzake Kajala Masanja kwa kujua ipo siku na yeye atakuwa na tatizo na atahitaji msaada kutoka kwa wengine.

“Unajua matatizo kaumbiwa binadamu na yakimfika mwenzako usifurahie bali sikitika pamoja nae lakini kama unaweza kumsaidia ni vizuri ukamsaidia kama ukishindwa sikitika pamoja nae na ndio maana nimefanya yote kwa pamoja kusikitika pamoja nae na kumsaidia pia”alisema Wema.

Kauli ya Wema imekuja kufuatia kutoa kiasi cha zaidi ya Shilingi Za kitanzania milioni 10 kama faini ya muigizaji mwenzxake Kajala Masanja ambaye alishitakiwa pamoja na mumewe walisomewa hukumu yao jana kwenye mahakama ya hakimu mkazi Kisutu Jijini Dar es Salaam.

Katika hukumu hiyo muigizaji huyo alihukumiwa kwenda jela miaka mitano au kulipa faini ya shilingi milioni 13, na mumewe kwenda jela miaka saba au kulipa faini ya shilingi milioni 200.

Pamoja na wasanii wa Bongo movie kuchangishana fedha kwa ajili ya kumtolea faini msanii huyo Wema Sepetu aliondoka mahakamani hapo na kwenda benki kuchukua fedha hizo na kuzitoa.

Kabla ya hukumu hiyo Kajala na mumewe Faraja Chambo walikuwa wanakabiliwa na makosa matatu ambayo ni pamoja na kula njama za kuhamisha umiliki wa nyumba iliyopo Kunduchi Salasala Jijini Dar es Salaam, huku ikiwa chini ya Taasisi ya kuzuia na kupambana na Rushwa (TAKUKURU).

Kosa la pili ni mnamo Aprili 14 mwaka 2010 walihamisha isisvyo halali umiliki wa nyumba hiyo kinyume na kifungu cha 34(2)A(3) cha Sheria ya kuzuia kuzuia na kupambana na Rushwa ya mwaka 2007, na shitaka la tatu ni la kutakatisha fedha ambalo walilitenda Aprili 14 mwaka 2010,huku wakijua ni kinyume cha Sheria.