Mzee Jangala: Msinibeze, nautaka urais

> Mwigizaji mkongwe nchini Bakari Malembela maarufu kama Mzee Jangala.

Muktasari:

Tamasha hilo litafanyika Juni 13 kwenye Uwanja wa Taifa na Makamu wa Rais, Dk Mohamed Gharib Bilal amealikwa kuwa mgeni rasmi.

Dar es Salaam. Mwigizaji mkongwe nchini, Bakari Mbelemba, maarufu kwa jina la kisanii la Mzee Jangala, amesema atatumia Tamasha la Ngoma za Asili “kutangaza nia ya kugombea urais” wa Jamhuri ya Muungano.

Tamasha hilo litafanyika Juni 13 kwenye Uwanja wa Taifa na Makamu wa Rais, Dk Mohamed Gharib Bilal amealikwa kuwa mgeni rasmi.

Akizungumza na gazeti hili kwenye ofisi za gazeti la Mwananchi jana, Mzee Jangala alisema ana haki na sifa zote za kugombea nafasi hiyo ya juu, kama waliotangulia kutangaza nia na kuwataka wananchi kutombeza kwa uamuzi wake.

Mzee Jangala, ambaye mara nyingi huigiza kama mzee mbishi na mwenye kauli za vichekesho, amesema Watanzania hawana budi kusubiri kusikia sera zake na mikakati yake endapo akifanikiwa kupata nafasi hiyo.

“Nimepanga kutangaza nia ya kugombea urais siku hiyo kwenye Uwanja wa Taifa mbele ya Makamu wa Rais Dk Mohammed Gharib Bilal, ambaye atakuwa mgeni rasmi katika tamasha la kihistoria la ngoma za asili,” alisema Mzee Jangala.

“Najua watu watafikiria natania katika jambo hili. Lakini siko hivyo. Nina uhakika na ninachokisema kwani ni haki ya kila raia na inatambulika kikatiba kugombea nafasi hii nyeti endapo tu ukiwa unazo sifa na vigezo,” alisema Mzee Jangala.

Msanii huyo mkongwe, ambaye hakutaja atagombea kwa chama gani, alisema kilichomsukuma kutangaza nia kwanza ni mzalendo na mapenzi kwa nchi yake.

“Pili ni kuondoa tatizo la mmomonyoko wa maadili kwa baadhi ya viongozi waliopewa dhamana na wananchi,” alisema msanii huyo aliyeanzia katika uigizaji wa jukwaani.

Alisema baadhi ya viongozi wakipewa madaraka wanasahau walikotoka na kutenda mambo kinyume na matarajio ya wananchi. Hali inayosababisha shughuli wanazozifanya kutofanyika ipasavyo na kuibua minung’uniko.

“Hawa tuliowachagua, baadhi yao hawana uchungu na nchi hii ndiyo maana rushwa imekuwa sehemu ya maisha yetu, kwa sababu walioko madarakani wapo kwa masilahi yao binafsi na si ya Watanzania,” alisema Mzee Jangala.

“Rushwa imekuwa changamoto mojawapo, sasa basi mimi nina uwezo, najiamini kuongoza na kupambana na jambo hili. Kinachohitajika kwa Watanzania kuniunga mkono pindi nitakapotangaza nia yangu.”

Hata hivyo, Mzee Jangala hakuwa tayari kutaja vipaumbele vyake endapo atapata nafasi ya kugombea urais akisema kuwa bado ni mapema sana. Ukizingatia kuna wimbi kubwa la Watanzania wanaotarajia kutangaza nia ya nafasi hiyo.

Pia, aliwataka wananchi kuachana na fikra kuwa mwaka huu nchi hii kiongozi anatakiwa kuwa kijana hata wazee wana uwezo, kinachohitajika ni sifa na hekima.

“Urais hauna kijana wala mzee kinachohitajika ni je? Una sifa na uzalendo kutoka moyoni. Sitaki ubunge nia yangu ni kuwasaidia Watanzania endapo nikapata ridhaa ya kuongoza nchi kupitia nafasi ya urais,” alisema Mzee Jangala ambaye ni mshindi wa Tuzo ya Mafanikio ya Muda Mrefu Katika Fani.

alifanikiwa kunyakuwa tuzo ya maisha kutokana na mchango wake mkubwa katika sanaa ya filamu na vichekesho, kutokana na uchapakazi na hekima aliyonayo.