Vibali vyampa changamoto Ali Kiba

Muktasari:

Meneja huyo, Aidan Seif alisema video hiyo ipo katika matengenezo nje ya nchi.

“Awali tulikuwa tumepanga ifanyike Afrika Kusini, lakini kutokana na machafuko tuliahirisha, ikatakiwa ifanyike nchi nyingine Afrika. Kilichochelewesha kwa sasa ni upatikanaji wa vibali kuingia Marekani kwa ajili ya shoo na mambo mengine, lakini tumeshafanikiwa kukamilisha taratibu hizo na wiki hii itafanyika,” alisema Aidan akiashiria kuwa picha za video hiyo zitachukuliwa Marekani.

Dar es Salaam. Kitendawili kilichokuwa kikiwaumiza vichwa mashabiki wa Ali Kiba, kimeteguliwa na meneja wake baada ya kuweka hadharani sababu ya kuchelewa kutengenezwa wa video ya wimbo wa “Cheketua” ya msanii huyo nyota.

Meneja huyo, Aidan Seif alisema video hiyo ipo katika matengenezo nje ya nchi.

“Awali tulikuwa tumepanga ifanyike Afrika Kusini, lakini kutokana na machafuko tuliahirisha, ikatakiwa ifanyike nchi nyingine Afrika. Kilichochelewesha kwa sasa ni upatikanaji wa vibali kuingia Marekani kwa ajili ya shoo na mambo mengine, lakini tumeshafanikiwa kukamilisha taratibu hizo na wiki hii itafanyika,” alisema Aidan akiashiria kuwa picha za video hiyo zitachukuliwa Marekani.

Alifafanua kwamba taratibu mbalimbali zinaendelea, hivyo kesho (Alhamisi) atazungumza jambo kuhusu hatima ya video hiyo na ni lini hasa itatolewa.

Mwanzoni mwa wiki, mashabiki mbalimbali wa Ali Kiba walianza kuhoji kupitia picha aliyoiweka nyota huyo wa muziki wa kizazi kipya katika mtandao wa kijamii wa instagram wakilalamikia ucheleweshwaji wa video hiyo na kudai kwamba anawaangusha.

“Kuna kitu watu wanashindwa kukikubali hapa. Ali Kiba anakabiliwa na pressure hii sababu ya kushindanishwa na Diamond. Mimi si muumini wa hizi team, lakini kama mchambuzi wa muziki na mtu ninayefuatilia sana muziki wa Tanzania, napenda watu watambue na kukubali kuwa Diamond na Ali Kiba hawako sawa tena. Mnamuonea tu Kiba kumfananisha na Diamond,” aliandika shabiki mmoja anayetumia jina la Kyusho katika mtandao huo.

“Hebu fikirieni mwenzie baada ya kutoa video ya wimbo wa “Nasema Nao”, ametoa video nyingine mbili tena akiwa na wasanii wakubwa Afrika na “Nakupenda” aliyorekodi na Iyanya, lakini Kiba bado anadaiwa video moja tu ya “Cheketua”. Ni kweli anawaangusha sana mashabiki wake, lakini pengine huo ndiyo uwezo wake hivyo kwa kumtegemea afanye kama Diamond mnamuonea tu!”