Wema Sepetu sasa rasmi katika siasa

Miss Tanzania 2006, Wema Sepetu  pichani kushoto akiwa na mama yake.

Muktasari:

Wema alisema kwa muda mrefu marehemu baba yake Balozi Issac Sepetu, alikuwa akimshauri aingie kwenye siasa na sasa ametimiza ndoto za wazazi wake.

Dar es Salaam. Miss Tanzania 2006, Wema Sepetu (pichani kushoto akiwa na mama yake), ametangaza rasmi nia yake ya kutaka kugombea ubunge wa Viti Maalumu Singida Mjini, kupitia tiketi ya CCM.

Wema alisema kwa muda mrefu marehemu baba yake Balozi Issac Sepetu, alikuwa akimshauri aingie kwenye siasa na sasa ametimiza ndoto za wazazi wake.

Miaka mitano iliyopita, Wema anayekubalika na mashabiki wengi, aliwahi kuweka wazi kuwa yeye ni mkereketwa wa Chama cha Mapinduzi (CCM) na mshabiki wa klabu ya soka ya Yanga na kwamba hiyo ndiyo sababu ya yeye kupendelea rangi za njano na kijani.

Akizungumza na kipindi cha redio cha Ala za Roho kwa njia ya simu, usiku wa kuamkia jana, Wema alisema yupo mkoani Singida kwa muda sasa akiendelea na kampeni ili kujitayarisha kuchukua fomu ifikapo Julai 15 mwaka huu.

Alisema anaamini nguvu za Mungu, Watanzania na watu wa Singida watamwamini na kumpa kura zao kwa kuwa sasa ni wakati wa vijana kujipambanua na kusaidia jamii yao.

“Nipo Singida kuhamasisha vijana wajitokeze kujiandikisha katika Daftari la Kudumu la Kupiga Kura, pia huku mimi ni nyumbani na nimejiandikisha tayari, ili ifikapo Julai 15 nichukue fomu. Ninachotafuta ni kuungwa mkono na Watanzania,” alisema Wema.

Alibainisha kuwa anajiamini na hakuna kitakachomshinda, kwani alipoingia katika mashindano ya ‘Miss Tanzania hakutegemea kama ataweza, lakini alifanikiwa, hata alipojitosa kwenye uigizaji akafanikiwa.

“Sasa naingia katika siasa, najua kwamba nitaweza. Mimi ni binadamu, nina mambo yangu, ila naamini hakuna linaloshindikana. Nitagombea ubunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Singida, Inshallah tuombe uzima,” alisema.

Wema alisema kwamba tayari ana kikundi chake cha kampeni akiwamo meneja wake Martin Kadinda sanjari na Petitman Wakuache.

“Nimeshafanya mengi kuhusu kujiandaa na uchaguzi hata kampeni, nilikuwa nazungumza na uongozi wangu ambao yupo Martin Kadinda pia yumo Petiman, huyu anahusika na kampeni yangu kwa hiyo Watanzania wajue tu kwamba nitachukua fomu ya kugombea ubunge wa Viti Maalumu na tutaona huko mbele itakavyokuwa kwa sababu hiki ni kinyang’anyiro,” alisema Wema.

Wema alisema kwamba kwa sasa ni kama anaingia kwenye mapambano yaliyo sawa na vita hivyo kuna kupata na kukosa.

“Lakini sifikirii kukosa kwa sababu mtu ukifikiri kukosa unajiweka kwenye ‘negative side’, lakini najua kwa nguvu za Watanzania na kwa nguvu za wananchi wa Singida, wataniamini na kunipa kura zao,”alisema.

Wema alifafanua kwamba licha ya kuungwa mkono na wanaume wengi mkoani humo, kinamama wa Singida pia wanamuunga mkono kwani wanamfahamu vizuri na sera zake wanazijua, hivyo ahofii kelele za watu wa pembeni.

“Nitaingia bungeni kwa ajili ya maslahi ya wananchi na kutetea haki za wananchi wangu, si kingine. Wamejitokeza watu wengi kwa ajili ya kugombea, kwa nini amejitokeza Wema Sepetu na watu wameanza kuzungumza mambo mengi?” alihoji.

Katika mahojiano hayo Diva alimuuliza Wema Sepetu kuhusu taarifa ya kuwa na uhusiano na rafiki wa kiume wa Linah alisema:

“Huwezi kuamini, habari hizo siyo za kweli kwa sababu tulikuwa tunafanyakazi naye tu, ila nimeshangazwa kuona kwa nini Linah ameenda hewani kwenye kipindi na kuzungumza hizo habari, naomba watu waelewe kwamba si kweli.”