Ben Pol: Sijajua bado nimshabikie nani kisiasa

Mwimbaji wa r&b nchini Ben Pol

Muktasari:

Ben Pol anayetamba na wimbo “Sophia” amesema wakati wasanii wengine wakijivika magwanda ya vyama, yeye amejiweka pembeni akitafakari, kwani anahisi hafai kufuata mkumbo ila moyo wake unaamua nini kwa mustakabali wa taifa lake.

Dar es Salaam. Tofauti na wasanii wengine ambao tayari wamejipambanua kisiasa, mwimbaji wa r&b nchini Ben Pol ana fikra tofauti na wenzake wengi, baada ya kuweka wazi kilichoujaza moyo wake kuhusu siasa.

Ben Pol anayetamba na wimbo “Sophia” amesema wakati wasanii wengine wakijivika magwanda ya vyama, yeye amejiweka pembeni akitafakari, kwani anahisi hafai kufuata mkumbo ila moyo wake unaamua nini kwa mustakabali wa taifa lake.

Akizungumza na Mwananchi jana, Ben Pol aliweka wazi kwamba kinachoendelea katika kampeni za Uchaguzi Mkuu kwa sasa kinamfanya afikirie zaidi ya mara mbili, iwapo wasanii wenzake na vijana wanaotumika kisiasa kama wanajua wanachokifanya na iwapo wamesoma kwa uhakika ilani za vyama wanavyoshabikia.

Alisema kubwa kwake ni sera za wagombea huku amani na utulivu wa nchi ni vitu anavyoomba usiku na mchana viendelee hata baada ya Oktoba 25.

“Kura yangu ina thamani kubwa, mashabiki wengi pia wananiuliza kwanini siweki chochote katika kurasa zangu za mitandao ya kijamii au kujumuika na wengine katika kampeni, mimi ni msanii na mfanyabiashara siwezi kuchanganya mambo. Lakini kubwa zaidi bado nafikiria nani nimpe kura yangu na naendelea kufuatilia ilani za vyama na vipaumbele vyao ili nijue nafanya nini Oktoba 25,” alisema Ben Pol.

Alisisitiza kuwa vijana wanatakiwa kutulia na kutafakari kwa makini, kabla hawajaamua kupiga kura na watakayemchagua atafanya nini na nini.

“Vijana wengi wanatumika, msikilize mgombea sera zake na tafakari kwa kina na namna atakavyoweza kuzitekeleza, ukiridhika kampigie kura,” alisema Ben Pol.