Bright

Muktasari:

  • Huyu ni Rashid Said lakini kwenye gemu la muziki anafahamika kwa jina la ‘Bright’.

Umahiri wa kuandika mashairi yake haukuanza jana wala juzi. Waliosoma naye shule ya msingi wanaufahamu uwezo wake kwani aliandika nyimbo nyingi zilizotumika kufundishia.

Huyu ni Rashid Said lakini kwenye gemu la muziki anafahamika kwa jina la ‘Bright’.

Msanii huyo anasema kazi hiyo ya kuandika mashairi aliianza tangu akiwa darasa la nne katika Shule ya Msingi Riyama na aliifanya vyema zaidi kutokana na kupenda somo la Stadi za Kazi, ambapo walikuwa wanajifunza sanaa na uchoraji.

“Yaani huwezi amini hata walimu walikuwa wakinitumia niwaandikie mashairi ya kufundishia darasani, pia nilikuwa nategemewa katika kutunga nyimbo za shule hususan kunapokuwa na hafla mbalimbali,” amesema.

Kuhusu alivyoingia kwenye muziki, amesema ilikuwa ni baada ya kumaliza kidato cha nne mwaka 2006, ambapo msanii Belle 9 ndiye waliyemuibua kutoka Ifakara mkoani Morogoro alikozaliwa na kukulia na kuja kufanya naye wimbo Dar es Salaam wa Nimemuona.

Baada ya hapo, Bright anasema aliendelea kuachia vibao vingine ikiwemo Nitunzie alioufanya na Baraka Da Prince na Umebadilika alioufanya na Nandy.

Kitu gani kilimvutia kuingia kwenye muziki? Bright anabainisha kuwa moja ya vitu vilivyomvutia kuingia kwenye sanaa ya muziki ni wimbo wa Presha ulioimbwa na wasanii Banana Zorro na Hafsa Kazinja.

Bright anasema ni kutokana na wimbo huo amejikuta akishawishika kutoa wimbo wa Umebadilika alioufanya na Nandy ambao unafanya vizuri hadi sasa.

Kama haitoshi anasema mbali na kutoa wimbo huo, pia ana mpango wa kufanya kazi na Banana Zorro ili aweze kukata kiu ya mapenzi aliyo nayo juu ya mwanamuziki huyo.

“Kwangu kwa kweli ukiniuliza mwanamuziki ninayempenda, simuoni mwingine zaidi ya Banana kwani ndiye kati ya watu walionivutia niingie kwenye muziki na nimeshajipanga kufanya naye kazi,” anasema Bright mwenye umri wa miaka 24.

Akieleza watu waliomsaidia kufika kimuziki hadi hapo alipo, anamtaja Belle 9 na kundi lao ambalo walimtoa wilayani Ifakara mkoani Morogoro na kuja kutengeneza naye wimbo wa Nimemuona jijini Dar es Salaam.

Baada ya hapo, Bright anasema aliendelea kuachia vibao vingine ikiwemo Nitunzie alioufanya na Baraka Da Prince na Umebadilika alioufanya na Nandy.

Nyingine ni Subira, Ni Wewe na Sina aliouachia mwezi uliopita ambao umeonyesha kufanya vizuri kwa kuwa mpaka sasa hivi umeshapata watazamaji zaidi ya 146,000 kwenye mtandao wa Youtube.