Millen Magese amuonyesha mtoto wake kwa mara ya kwanza

Muktasari:

  • Millen wakati huo akijulikana kwa jina la Happiness aliwahi kutwaa taji la Miss Tanzania akitokea Miss Temeke

Hatimaye  mwanamitindo  Millen Magese’, amemuweka wazi mtoto wake kwa mara ya kwanza  leo Machi 16.

Mtoto huyo, alizaliwa Julai mwaka jana na akabatizwa jina la Prince Kairo Michael.

Millen au Happiness aliyewahi kuwa Miss Tanzania mwaka 2001 na baadaye kujikita katika uanamitindo, ameitupia picha hiyo jana kwenye ukurasa wake wa Instagram akimuonyesha na mwanae wakiwa wamevaa nguo nyeupe.

Picha hiyo pia imetumika kupamba Jarida la Genevieve la nchini Nigeria ambalo pia lina mahojiano maalumu kuhusu maisha yake na safari nzima ya yeye kupata mtoto.

Mrembo huyo aliisindikiza picha hiyo kwa maneno yaliyosema: “Nimeamua kuonyesha picha hiyo si kwa ajili ya mashabiki wangu na watu walionisaidia,  bali kueleza habari ya imani na matumaini ambayo itawasaidia wengine ambao wamekata tamaa katika kupata mtoto.”

Kwa nyakati tofauti Millen amewahi kusimulia na kumwaga machozi hadharani akielezea tatizo lake la kutoshika ujauzito kutokana na mirija yake kuziba tangu mwaka 2007.

 

Katika maelezo yake, alisema kuna kipindi alikata tamaa mpaka akajiandaa kuondoa kizazi na hapo ni baada ya kufanyiwa oparesheni zisizopungua 13 ambapo pamoja na hayo, aliambiwa moja ya tiba ya tatizo hilo liitwalo ‘Endometriosis’ kwa kizungu, ni kuzaa.

Kutokana na tatizo hilo, mwaka 2014 Millen aliamua kuanzisha mfuko kwa wanawake kwa ajili ya kutibu ugonjwa  ‘Endometriosis’ lengo lake likiwa kusaidia kuelimisha wanawake ili kujua dalili na matibabu ya ugonjwa huo.

Baadhi ya watu maarufu wametoa maoni yao baada ya kuachia picha hiyo akiwemo mrembo Wema Sepetu, ambaye amesema picha hiyo licha ya kumliza pia imempa matumaini na kumfanya kuendelea kusali akiamini na yeye ipo siku atapata mtoto.

Mwingine ni aliyewahi kuwa mshindi wa pili katika shinda la Miss Tanzania mwaka 2006, Jokate Mwegelo, ambaye alimsifia mtoto huyo  na kuomba Mungu aibariki familia ya Millen.