Uwoya, Dogo Janja hawajapelekana kwa wazazi

Muktasari:

Oktoba 28 mwaka jana wawili walifunga ndoa ya kimya kimya

Ikiwa imepita miezi mitano tangu wasanii Irene Uwoya na Dogo Janja wafunge ndoa,  Uwoya amesema ameshindwa kumpeleka Dogo kwa mama yake hadi leo kwa kile alichodai  kuwa mtu wa kusafiri mara kwa mara.

Oktoba 28 mwaka jana wawili hawa walifunga ndoa ya kimya kimya ambayo ilizua gumzo kutokana na kuwapo kwa utofauti mkubwa wa umri kati yao.

Hata hivyo, kwa kipindi chote hicho tangu waoane, Dogo Janja ndiye aliyekuwa muwazi kuzungumzia suala hilo, huku Uwoya akiwa anakwepakwepa mpaka pale walipoonekana kwa mara ya kwanza pamoja katika harusi ya Shilole.

Akihojiwa leo na kituo cha redio cha Clouds, amesema pamoja na kufunga ndoa huko bado hajampeleka Dogo kwao  kwa kuwa mama yake ni mtu ambaye anasafiri mara kwa mara huku akiahidi kuwa siku moja wataenda.

Wakati akisema hivyo kwa nyakati tofauti wazazi wa Uwoya akiwamo baba yake aliyewahi kuzungumza na gazeti hili amesema hawaitambui ndoa hiyo na wala hawaamini mtoto wao mpaka leo kama kaolewa na msanii huyo anayefanya vizuri katika muziki wa bongofleva.

Kuhusu kubadili dini kwa ajili ya kuolewa, Uwoya amesema ilikuwa ni uamuzi wake na haoni ubaya kwani katika familia yao pia kuna ndugu ambao ni Waislamu na hata jina la Sheila aliloamua kulitumia  alipewa na bibi yake hivyo haoni kama kuna shida.

 

Wivu wake kwa Dogo ni shida

Wakati Dogo akiwa anatesa na wimbo wake wa Wayuwayu aliouchia siku za karibuni na kuigiza kama mwanamke, Uwoya anadai kuwa yeye ndiyo sababu kwani hakutaka aigize na mwanamke mwingine.

Alipoulizwa kama itakuwa hivyo kwa nyimbo zake zote, mama huyo wa mtoto mmoja amesema watatumia hata ndugu zake au wa Dogo Janja kuliko kutumia watu tofauti asiowajua.

Kwa upande wa Dogo Janja amesema hana wivu wa hivyo kwa Uwoya na atakuwa tayari aigize na wanaume wengine kwani anaamini hiyo ni kazi na akwa asilimia 100 hawezi kumsaliti.