MwanzoContactsEmail
Home Biashara Biashara za Kitaifa 'Benki ziache kutoza riba kubwa'
BOOKMARK THIS PAGE
'Benki ziache kutoza riba kubwa'  Send to a friend
Wednesday, 20 April 2011 08:23

Raymond Kaminyoge
WAWEKEZAJI wamelalamika riba kubwa inayotozwa katika mikopo kwenye benki za Jumuiya Afrika Mashariki kwa kuwa zinakwamisha maendeleo ya kiuchumi hasa katika sekta ya kilimo.

Wawekezaji hao walisema benki zilizopo kwenye ukanda wa Afrika Mashariki zinatoza riba ya zaidi ya asilimia 20 na kusababisha wakulima washindwe kumudu mikopo hiyo.

Hamidu Mwakasaka alisema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati akichangia kwenye Jukwaa la Kimataifa la uwekezaji la Afrika lililoandaliwa na Baraza la Biashara la Jumuiya ya Madola.

Alisema pamoja na riba kubwa, pia wakulima wananyanyapaliwa kwa kutopewa mikopo na hali hiyo kukwamisha  maendeleo ya kilimo katika ukanda wa Afrika Mashariki.

“Benki hizo zipo kwa ajili ya kuwakopesha wafanyabiashara wanaouza bidhaa ambazo zimezalishwa, lakini kwa wazalishaji wenyewe ni vigumu kupata mikopo kutoka kwenye benki,” alisema Mwakasaka.

Hatua hiyo iliungwa mkono na Hassan Makini kutoka Burundi ambaye alisema inasikitisha benki zinatoza riba ya asilimia 25 na kutakiwa kurudisha mikopo hiyo kwa muda wa miaka mitatu tu.

“Mimi ni mkulima wa embe, ili niweze kuvuna nahitaji zaidi ya miaka minne, mkopo wa miaka mitatu ambao natakiwa kurudisha kwa riba utanisaidia kweli,” alisema.

Alisema serikali zetu ziwekeze kwenye kilimo kwa kuwa benki zetu zimeshindwa kufanya hivyo kwani ziko kibiashara zaidi kuliko kutoa huduma.

Akijibu hoja hizo katika Jukwaa hilo, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Equety Bank Ltd, Dk James Mwangi alisema serikali za Afrika Mashariki zinapaswa kuwekeza katika utoaji wa mitaji kwa wananchi wake.

“Kama serikali zinavyowekeza kwenye maji, elimu na afya, vilevile ifanye hivyo katika kuwawezesha wananchi wake kupata mitaji ili kuendeleza sekta mbalimbali kikiwemo kilimo,” alisema Mwangi.

Alisema benki pekee yake haziwezi kusaidia katika kutoa mitaji kwani zinaendeshwa kwa kufuata kanuni za kifedha walizowekwa ambazo si watu wote wanaweza kunufaika.

Mwangi alisema benki nyingi zinawakwepa wakulima kutokana na kuendesha kilimo  cha kutegemea mvua ambacho hakina uhakika.

“ Pia serikali zetu ziwekeze kwenye kilimo cha kisasa cha umwagiliaji ili kuwa na uhakika na hivyo kuaminiwa na benki zetu,” alisema Mwangi.

Jukwaa hilo limeandaliwa na Baraza la Biashara la Jumuiya ya Madola kwa kushirikiana na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC)

Add this page to your favorite Social Bookmarking websites
Reddit! Del.icio.us! Mixx! Free and Open Source Software News Google! Live! Facebook! StumbleUpon! TwitThis Joomla Free PHP
 

Comments 

 
0 #2 2011-04-20 11:47
Ukweli ni kwamba riba za hizi nchi ni kubwa sana.Sio kwa mkulima tu hata kwa mfanyabiashara anayeuza bidhaa zilizokamilika.Hua nashindwa kuelewa bank hua zinataka kuona wateja wao wakifilisika?
Ni vyema wakachukua riba kiasi ambayo itamwezesha mfanyabiashara kunufaika nao wandelee kukua.
Quote
 
 
0 #1 2011-04-20 09:50
asilimia 25 ni nyingi sana kwa mkulima ,mimi nafikiri mkulima hatapa faida ila bank ndiyo itakayonufaika .tunaomba wapunguze riba ,maana kila kazi anayofanya mtu kuna hasara na faida.ukimkopesha mtu ujue kuna hasara siyo kila mara faida tu.hata kama umepata hasara bank wanachojua ni marejesho yafanyike ,wao bank hawajui hasara,kwa vile hamjui hasara basi tunaomba riba ipungue.
Quote
 

Add comment

Tumia jukwaa ili kutoa maoni ambayo yatasaidia kulijenga taifa letu. Kumbuka, maoni yako yatapitiwa kwanza kabla hayajarushwa hewani!!!!!!


Banner
Banner