
| Tanesco wasitisha mgawo wa umeme | Send to a friend |
| Wednesday, 08 December 2010 20:58 |
Leon BahatiSHIRIKA la Umeme nchini Tanesco limesitisha mgawo wa umeme uliokuwa unaikumba nchi nzima. Meneja Mahusiano wa Tanesco, Badra Masoud aliwaambia waandishi wa habari kwamba wamesitisha mgao wa umeme baada ya jenereta za Songas ziliokuwa zimeharibika kutengamaa na kwamba vina vya maji vya mabwawa ya Kihansi na Mtera, vimeongezeka. Masoud alikuwa akizungumza na jopo la waandishi wa habari waliotembelea mitambo ya kuzalisha umeme ya Kihansi na Mtera ambako waliona jinsi umeme unavyozalishwa na matatizo yaliyoikumba shirika hilo. Shirika hilo, lilitangaza kuanza kwa mgawo wa umeme tangu Novemba 27, mwaka huu katika mikoa mbalimbali iliyounganishwa katika gridi ya taifa. Mgawo huo ulikuja wakati maeneo kadhaa jijini Dar es Salaam, yakikosa umeme kwa takribani wiki mbili kutokana na kuungua kwa transfoma ya Kipawa inayogawa umeme wa gridi ya taifa na kupungua kwa kina cha maji katika Bwawa la New Pangani na Kihansi Akizungumza jana akiwa Kihansi Badra alisema mvua ziizonyesha kwa siku mbili zimelipa bwawa hilo kiwango cha maji kinachoweza kuzalisha umeme nchini. Badra alisema mgawo ulisimamishwa tangu jana na hategemei hali hiyo kubadilika siku za karibuni kutokana na mvua kunyesha nchi nzima. Mgawo wa umeme ambao huo wa umeme uliodumu kwa karibu siku 20, uliathiri maeneo yote nchini ambayo yanahudumiwa na gridi ya taifa. Kaimu Meneja wa Kihansi, Patrick Lwesya alisema mvua zilizonyesha kwa siku mbili zimelipa bwawa hilo kiwango cha maji kinachoweza kuzalisha megawati 120, na jana megawati 75, zilizalishwa. Kabla ya maji kuongezeka Kihansi ilikuwa ikizalisha megawati 60. |



Leon Bahati










