
| Muswada wa madini waitoa jasho serikali | Send to a friend |
| Wednesday, 21 April 2010 23:20 |
Habel Chidawali na Frederick Katulanda, DodomaMUSWADA wa Sheria mpya ya madini unaendelea kuitoa jasho serikali baada ya jana kukwama kuwasilishwa bungeni kwa siku ya pili bila maelezo.Juzi Spika wa Bunge, Samuel Sitta aliwaeleza wabunge kuwa muswada huo ambao tayari umeleta mvutano mkubwa katika jamii ungewasilishwa jana baada ya kushindikana Jumatatu iliyopita lakini, tofauti na ahadi hiyo, haukuwamo kwenye ratiba ya shughuli za Bunge. “Niwaombe wabunge kuwa kesho (jana) tutajadili muswada wa sheria ya madini, niwaombe mkajiandae,” alisema Spika Sitta wakati wa matangazo ya mwisho kabla ya kuahirisha Bunge juzi. Lakini jana orodha ya shughuli za Bunge hazikuonyesha muswada huo na Spika baadaye aliwatangazia wajumbe wa Kamati ya Nishati na Madini mkutano baada ya kipindi cha maswali na majibu. Mbali na mkutano huo wa wajumbe wa Kamati ya Nishati na Madini, pia Spika Sitta alitangaza mkutano wa wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) baadaye jioni jana. “Leo muswada wa sheria ya madini hautawasilishwa kwa sababu hali bado ngumu sana, unaendelea kujadiliwa ili kuhakikisha ukiwasilisha haukumbani na upinzani na unapita kwa sababu hiki ni kipindi cha kuelekea uchaguzi,” alieleza mmoja wa wabunge ambaye hakupenda kuandikwa jina lake gazetini. Wabunge wengine waliozungumza na gazeti hili jana walisema kitendo cha serikali kushindwa kuwasilisha muswada huo ni dalili ya waziri mwenye dhamana kusoma alama za nyakati na kuugopa kukwama kuupitisha. "Waziri angelazimisha kuleta Muswada huo ni wazi kuwa angekutana na kiyama kama alichokutana nacho Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi ambaye wabunge walimgomea katika miswada yake miwili," mbunge mmoja ambaye hakutaka atajwe gazetini alisema. Wadau walianza kushikwa wasiwasi kuhusu muswada huo pale gazeti hili liliporipoti taarifa za ndani kwamba Rais Jakaya Kikwete ametoa maelekezo maalum kutaka muswada huo ujadiliwe kwa hati ya dharura. Mbali na wadau mbalimbali kupinga muswada huo waziwazi, Waziri na Kilimo, Chakula na Ushirika Stephen Wassira na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Ezekiel Maige waliupinga muswada huo hadharani wakati wa semina ya Kamati ya Madini iliyofanyika mjini hapa wiki iliyopita. Kitendo cha muswada huo kupingwa na viongozi wa dini na hata mawaziri kimeonekana kuistua serikali kiasi cha kusitisha kuwasilisha haraka hivyo kuamua kuutayarisha upya ili kukidhi mahitaji ya wengi. “Mwenyekiti wa Kamati ya Nishati na Madini ya Bunge, Shelukindo anawatangazia wajumbe wote wa kamati hiyo kuelekea katika kikao cha kamati katika Ukumbi wa Pius Msekwa kuanzia majira ya saa 5 asubuhi,” alisema spika Sitta na kuongeza; “Nyaraka za sera za madini ziko tayari zimewekwa katika masanduku yenu, naomba mzichukue na kuzisoma kwa makini waheshimiwa wabunge.” Jana ilikuwa siku ya pili kwa Kamati ya Nishati na Madini kukutana baada ya juzi kutwa nzima wajumbe wake kuendeleza majadiliano hayo hadi usiku jambo linaloonyesha kuwa bado ngoma ni nzito. Mwenyekiti wa Kamati ya Nishati na Madini William Shelukindo jana alijifungia na kamati yake na kila alipopigiwa simu ya mkononi iliita bila mafanikio muda wote. Hata hivyo, Shelukindo aliwahi kukaririwa akisema kamati hiyo haitaweza na wala haithubutu kupitisha vitu ambavyo vinaopnekana wazi kuwa na utata na ambavyo havitakuwa na tija kwa Watanzania. Kwa mujibu wa ratiba ya Mkutano wa Bunge unaoendelea mjini hapa, sheria hiyo ilipaswa kuwasilishwa bungeni tangu siku ya Jumatatu ambapo ungejadiliwa kwa siku mbili hadi jana, lakini haikuweza kuwasilishwa. Mwishoni mwa wiki Wizara ya Nishati na Madini iliitisha semina katika Ukumbi wa Pius Msekwa ambapo wabunge pamoja na wadau wa madini walionyesha nia ya wazi kuwa walitaka kuukwamisha muswada huo. Katika semina hiyo, mawaziri wawili walionyesha wazi kuwa walikuwa wanapingana na serikali kuwa hawangekuwa tayari kuunga mkono muswada huo kwa kuwa ulikuwa ukiwakandamiza wananchi. Jana Waziri wa Kilimo na Chakula, Stephen Wasira aliliambia Mwananchi kuwa kupinga kwake muswada hakuwa akiikomoa serikali kama alivyoripotiwa katika katika vyombo vya habari bali ilikuwa ni makusudi mazima ya kumsaidia waziri mwenzake. “Mimi sikuwa napinga muswada hata kidogo kama watu wanavyosema, lakini nilikuwa na kila sababu kwa kuwa nilikuwa namsaidia Waziri mwenzangu pamoja na Watanzania wote ambao wanaguswa katika sekta hiyo,” alisema Wasira. Kuhusu baadhi ya watu kumtaka ajiuzulu wadhifa huo kutokana na mabishano hayo Wasira alisema “Sina cha kusema” hata alipotakiwa kuendelea kuzungumza zaidi aliondoka na kumuacha mwandishi. Hata hivyo, baadhi ya watu wanaonekana kuwatetea mawaziri hao wakisema kuwa ilikuwa ni haki yao na kwamba hawatakiwi kuhukumiwa kwani mabishano yao yalikuwa kwenye semina na sio ndani ya kikao halali. Kabla ya hapo walishakaa wabunge tena ambapo waliweza kulumbana bila ya mafanikio kwani taarifa za ndani ya kikoa hicho zilidai kuwa kulikuwa na malumbano makali jambo lililothibitishwa na mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe. “Ni kweli tulikuwa na malumbano makali sana, lakini ni ya kawaida tu wala sio jambo la kutisha maana kitu kinachogusa masilahi ya nchi hatuwezi kukipitisha hivi hivi tu,” alisema Ziito wakati akizungumza Mwananchi katika viwanja vya Bunge juzi. Hata hivyo, habari zilizolifikia Mwananchi kutoka kwa mmoja wa wabunge ambaye ni mdau wa kutoka katika maeneo yanayozalisha madini alisema kuwa muswada huo unatarajia kuwasilishwa siku ya Ijumaa jambo linaloonyesha kuwa wabunge watakuwa wamenyimwa nafasi ya kuchangia. Siku ya Ijumaa ilikuwa na ratiba za wabunge kupkiea Taarifa za kamati ya Miundombinu kuhusu Azimio la Bunge kuhusu Utendaji wa kazi usioridhisha wa kampuni ya Tanzania International Container Terminal Services (TICTS) pamoja na Uendeshaji usioriudhisha wa Shirika la Reli Tanzania uliofanywa na Kampuni ya RITES ya India Mambo mengine yaliyotarajia kuwasilihwa siku hiyo yaliwasilishwa jana ambayo ni pamoja na taarifa za Hesabu za serikali za Mitaa,Serikali Kuu pamoja na Hesabu za Mashirika ya Umma ambazo zote ziliwasilishwa jana. |
| Last Updated on Thursday, 22 April 2010 23:27 |



Habel Chidawali na Frederick Katulanda, Dodoma








