CWT Arusha yahofia uhakiki wanafunzi hewa
Muktasari:
Akizungumza ofisini kwake jana, Kaimu Mwenyekiti wa CWT Mkoa wa Arusha, Andrew Ngazu alisema chama kinamtaka mkurugenzi wa jiji kurudia uhakiki kwa sababu uamuzi uliotolewa ulikuwa wa binafsi na haukufuata utaratibu maalumu.
Arusha. Chama cha Walimu Tanzania (CWT) Mkoa wa Arusha, kimetaka uhakiki wa wanafunzi hewa jijini hapa kuanza upya kwa madai ya uwapo wa uamuzi wa chuki dhidi ya wakuu wa shule.
Akizungumza ofisini kwake jana, Kaimu Mwenyekiti wa CWT Mkoa wa Arusha, Andrew Ngazu alisema chama kinamtaka mkurugenzi wa jiji kurudia uhakiki kwa sababu uamuzi uliotolewa ulikuwa wa binafsi na haukufuata utaratibu maalumu.
“Tunamuunga mkono Rais Johh Magufuli kuhakiki shule zenye wanafunzi hewa, ila tunapinga kwa nguvu zote uhakiki uliofanyika Arusha,” alisema Ngazu na kuongeza: “Tunaamini umefanywa na maofisa wa elimu kwa chuki dhidi ya walimu wa shule, hali iliyosababisha kuonewa kwa baadhi ya walimu huku shule zenye wanafunzi hewa zikiachwa.” Kaimu Katibu wa CWT, Nurueli Kavishe alisema mpaka sasa wana ushahidi unaojitosheleza kuwa mwajiri wao ambaye ni mkurugezi wa jiji hakutumia takwimu zilizopo.
Katibu wa CWT Wilaya ya Arumeru, Joyce Kizaji aliwataka wakurugenzi kuacha kuwatisha walimu kuhusu Mwenge kwani siyo lazima.