Maskauti watakiwa kudumisha amani

Muktasari:

  • Balozi Seif amesema Chama cha Maskauti kimefikisha miaka 100 tangu kuzaliwa kwake kutokana na umoja walionao na kuwaasa kuulinda umoja huo.

 

Makamu wa Pili wa Rais katika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), Balozi Seif Alli Iddi amewataka maskauti nchini kudumisha amani kwa sababu ikikosekana huleta chuki, visasi, maradhi na uharibifu.

Akizungunza wakati wa ufungaji wa maadhimisho ya miaka 100 ya Chama cha Maskauti Nchini yaliyofanyika katika Ukumbi wa Chimwaga mjini hapa leo, Balozi Seif amesema vijana ni mhimili mkubwa wa kuilinda amani na wakiyumba nchi nayo itayumba.

"Hivyo vijana muwe mstari wa mbele kuhakikisha kuwa mnailinda amani kwa kuhakikisha kuwa hakuna vurugu," alisema na kuwataka kuwa wamoja, waadilifu na wazalendo.

Balozi Seif amesema chama hicho kimeweza kufikisha miaka 100 tangu kuzaliwa kwake kutokana na umoja walionao ambao umejenga uimara licha ya changamoto mbalimbali.

"Umoja wenu ndio utakaowaimarisha hakikisheni mnaulinda kwa gharama yoyote ili kujenga skauti imara na inayoheshimika duniani kote,"amesema.

Pia aliwataka maskauti hao kujifunza kuogelea na kupiga mbizi ili waweze kufanya uokozi katika maji na kuwaokoa wenzao watakaopata bahati mbaya ya kuzama kwenye maji.

Rais wa chama hicho na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako aliwataka maskauti hao kwenda kuyatumia waliyofundishwa na kuwafundisha wengine.

"Mafunzo haya yametolewa na viongozi mbalimbali, yakiwamo ya vita dhidi ya rushwa ambayo imekuwa ni kansa nchini na kulitafuna Taifa, mmepata mada kutoka Takukuru (Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa) na mafunzo yawe chachu katika maisha yenu,"amesema.

Amesema maskauti hao walijifunza kuhusu dawa za kulevya, mmomonyoko wa maadili, uvunjifu wa mabaadili, ubadhilifu, mazingira ya ujasiri, uokoaji katika majanga, mazingira na uzalendo.

Mwenyekiti wa Bunge Mussa Zungu aliyemwakilisha Spika wa Bunge, amesema nchi imeingia katika vita kubwa ya uchumi hivyo maskauti hao wana jukumu la kwenda kuwaambia wenzao watakaporudi majumbani mwao kuunga mkono juhudi za Rais John Magufuli za mapambano hayo.

"Nyie muwe mawakala wa kuitangaza mitaani majumbani kuzaliwa kwa Tanzania mpya," amesema Zungu ambaye pia ni mbunge wa Ilala (CCM).

Katika mkusanyiko huo wa siku tisa uliowakusanya maskauti 4100 kutoka mikoa yote nchini, Shirika la AAR Healthcare kupitia mradi wa T4H ilitoa vidonge vya minyoo kwa maskauti hao.