...Muhimbili yafanunua kilichomuua Salum Kindamba

Dar es Salaam. Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) imetoa ufafanuzi kuhusu kifo cha Salum Kindamba anayedaiwa kuuawa na polisi.

Familia ya Kindamba ililalamikia utata wa ripoti ya Muhimbili kuhusu chanzo cha kifo cha ndugu yao huyo wanayedai alipigwa risasi Agosti 11, akiwa baa eneo la Jet Rumo, Dar es Salaam.

Kaka wa marehemu, Omary Kindamba alisema walishangaa kupewa kibali cha mazishi Muhimbili kinachoonyesha kuwa Salum alifariki dunia kwa mshtuko wakati polisi wanasema alichomwa na kitu chenye ncha kali.

Familia hiyo ilisema juzi kuwa, itaendelea kuuacha mwili huo mochwari hadi itakapopata ukweli kuhusu chanzo cha kifo cha ndugu yao.

Hata hivyo, jana Mkuu wa Kitengo cha Uchunguzi wa Magonjwa cha MNH, Dk Praxeda Ogweyo alisema ripoti yao inaonyesha kwamba Salum alifariki kutokana na mshtuko uliosababishwa na kuvuja damu nyingi kwa sababu ya majeraha ya risasi.

“Ndiyo maana hatuwezi kuandika sababu ya kifo ni mshtuko halafu tukaishia hapo, haiwezekani. Mshtuko unaweza kusababishwa na vitu vingi, kwa mfano akivuja damu sana tunasema amefariki kwa mshtuko uliosababishwa na kuvuja damu kwa wingi,” alisema Dk Ogweyo ambaye kitengo chake pia kinashughulika kitabibu na uchunguzi wa sababu za vifo.

Alisema mfano kama mtu amepigwa risasi ikasababisha majeraha makubwa kama ilivyokuwa kwa Salum, ripoti inaandikwa kuwa amefariki dunia kwa mshtuko uliosababishwa na kuvuja damu kwa wingi kutokana na jeraha lililosababishwa na kitu chenye ncha kali.

“Ripoti ya postmortem (uchunguzi wa mwili wa marehemu) iliyoandikwa kwenye form ya polisi MFL.1 imeonyesha matokeo ya vitu vyote alivyoona mchunguzi kwenye mwili wa marehemu ambavyo hatuwezi kuviweka hadharani au gazetini,” alisema.

Aliongeza kuwa, “Hiki kifo hicho ni cha ghafla na kinachunguzwa na polisi na ndiyo maana ukafanyika uchunguzi wa kitabibu wa mwili wa marehemu.”

Akizungumzia ufafanuzi huo, kaka wa marehemu, Omary alisema wameambiwa na polisi kituo cha Chang’ombe walikofungua malalamiko yao kuwa, watapewa ripoti kamili ya uchunguzi wa hospitali kesho.