Sunday, August 13, 2017

Wafanyakazi wa Sadolin wahofia kupunguzwa

By Raymond Kaminyoge,Mwananchi rkaminyoge@mwananchi.co.tz

Wafanyakazi wa iliyokuwa Kampuni ya Rangi ya Sadolin Paint Ltd hawatapunguzwa kazi licha ya kampuni hiyo kuuzwa.

Kampuni hiyo imeuzwa kwenye kampuni ya Kansai Plascon ya Japan.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Kansai Plascon Tanzania, Amin Habib amesema kampuni hiyo imenunua shughuli zote za rangi za Sadolin nchini.

“Tunaanza kutumia nembo ya Kansai Plascon katika rangi iliyokuwa ikijulikana kama Sadolin, tumefurahi kupata teknolojia hii na tutaiongezea ubora,” amesema.

Kuhusu wafanyakazi, Habib amesema wafanyakazi wote pamoja na menejimenti wataendelea kama kawaida na hakuna kitakachobadilika.

Awali wafanyakazi wa Kampuni ya Sadolin walikuwa wakihofia kwamba kuuzwa kwa kampuni hiyo huenda kukasababisha wao kupunguzwa kazini.

“Kitakachobadilika hapa ni nembo lakini rangi hii yenye nembo mpya itaongezewa ubora na teknolojia mpya,” amesema.

Habab amesema mawakala, wasafirishaji na maduka yataendelea kuwa yaleyale yaliyokuwa yakitumiwa na Sadolin.

Amesema kwa Tanzania, Kansai Plascon imewekeza Dola za Marekani milioni 15 sawa na Sh33 bilioni.

Kuhusu teknolojia, Habib amesema kampuni hiyo itaanza kuuza rangi ambayo ikipakwa majumbani itasaidia kuua mbu na wadudu wengine.

Amesema kabla ya kuanza kuuza rangi hiyo, wamepeleka maombi wizara ya Afya na Mkemia wa Mkuu wa Serikali ili kupata kibali cha kuanza kutengeneza rangi hiyo.

“Rangi hii imeanza kutumika katika baadhi ya nchi tukipata kibali tutaanza kuitengeneza hapa Tanzania, tunatarajia baada ya miezi sita tutaanza kazi hiyo,” amesema.

Amesema malaria bado ni tatizo katika baadhi ya jamii hapa nchini hivyo teknolojia hiyo itasaidia katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa malaria

Kwa upande wake, Rais wa Kansai Plascon wa Afrika Mashariki, Gary Van der Merwe amesema kwa kuwa Sadolin ilikuwa ikijiendesha kwa ufanisi, mkakati uliopo ni kuboresha zaidi.

“Tutafanya kazi ya kupanua zaidi teknolojia iliyopo ili kuwapa wateja wetu rangi za kiwango cha juu zaidi katika soko,” amesema.

 

-->