‘Mke wangu anapoteza fahamu mara kwa mara’

Bi Amina Mohamed akizungumza na mwandishi wa gazeti hili kuhusiana na tukio la kufariki kwa wajukuu zake watatu kwa mara moja jijini Dar es Salaam.Picha na Tumaini Msowoya.

Muktasari:

Tukio la watoto watatu kupoteza maisha Oktoba 15, 2018 wakiwa ndani ya gari bovu limeendelea kumuumiza, Rukia Seif aliyepoteza watoto wawili ambaye amekuwa akipoteza fahamu mara kwa mara 

Dar es Salaam. Wiki moja tangu watoto watatu wa familia moja kupotea na kukutwa siku tatu baadaye wakiwa wamefariki dunia katika gari bovu, wazazi wa watoto hao wamesimulia tukio hilo huku mmoja akisema tangu wakati huo, mkewe amekuwa akipoteza fahamu mara kwa mara.

Watoto hao Jamila Mohamed (9), Amina Kunambi (7) na Yusuph Selemani (2), Oktoba 15 mwaka huu walikwenda kumtembelea babu yao, Seif Mayumba Mtaa wa Njaro wilayani Temeke jijini Dar es Saalam na baadaye wakatoka kwenda kucheza lakini hawakuonekana hadi Oktoba 17 asubuhi walipokutwa wamekufa kwenye gari.

Mayumba alitoa taarifa ya kupotea kwa wajukuu zake na waliwatafuta bila mafanikio lakini siku mbili tangu walipotoweka, alisikia harufu kali na alipofuatilia alibaini inatokea katika gari bovu aina ya Toyota Mark X na alipofungua mlango alikuta miili ya watoto hao.

Watoto hao waliokuwa wakiishi Mbagala, walizikwa katika makaburi ya Chang’ombe Alhamisi iliyopita.

Selemani Yusuph, baba wa watoto Yusuph na Jamila alisema licha ya kila mtu kuzungumza lake kuhusu vifo vya watoto wake, anamuachia Mungu.

Wapo walioshangazwa na kitendo cha watoto hao kushindwa kutoka katika gari hilo, ikiwa ni pamoja na kuvunja vioo.

“Kila siku ninapoondoka watoto wangu walikuwa wakiniagiza zawadi nawakumbuka sana. Kwa kweli inaumiza na imebaki simanzi lakini kazi ya Mungu haina makosa,” alisema Selemani.

Seleman akimzungumzia mkewe Rukia Seif, alisema amekuwa akipoteza fahamu kila anapowakumbuka watoto hao.

“Kazi niliyonayo ni kumsaidia mwenzangu apokee kilichotokea kwa sababu imeshakuwa. Tangu msiba utokee mke wangu amekuwa mtu wa kuzimia, tunachofanya ni kumsaidia arejee kwenye hali ya kawaida,” alisema Seleman.

Ilivyokuwa

Selemani alisema Jumatatu asubuhi mkewe aliomba aende nyumbani kwao Mtaa wa Njaro kuwasalimia wazazi wake lakini kwa sababu hakuwa na nauli alimzuia.

“Baadaye akanipigia simu kwamba ameamua kwenda nauli aliazima kwa jirani na mimi nikamueleza kuwa nikitoka kazini jioni nitawapitia,” alisema.

Alisema ilipofika jioni alipigiwa simu na kuelezwa kuwa watoto hawaonekani, “Nilijua ananitania lakini alinisisitiza kuwa watoto hawapo.

“Nilikwenda kwa wakwe zangu na siku hiyo tuliwatafuta bila mafanikio tukatoa taarifa serikali za mtaa, tulihangaika hadi usiku wa manane hakukuwa na taarifa yoyote.”

Alisisitiza, “Pale kwenye gari (Mark X) tulikuwa tunapita sana na mke wangu tukiwatafuta watoto kuna muda alipoteza fahamu kwenye eneo lilelile lakini akili ya kuangalia kwenye gari haikuwepo.”

Alisema siku ya tatu wakati wakiendelea kutafuta alipigiwa simu kuwa watoto wamepatikana lakini wamefariki.

“Nilikaa chini, nilihisi moyo unakimbia mbio nilichukua bodaboda hadi nyumbani nikaona watu wamezunguka gari,” alisema.

“Nilipofika nikazuiwa nisisogee nikawaambia mimi mzazi basi wakanisaidia nilisogea pale kweli sikuamini nilichokuwa nimekiona.”

“Tunajipanga upya na mke wangu, Mungu atatujalia watoto wengine Inshalah,” alisema.

Babu awalilia

Mayumba alisema wajuu zake walikuwa na tabia ya kwenda kucheza kwenye gereji anayolinda na siku hiyo aliwanunulia mkate na kuwaacha wakiwa wanakula.

“Niliporudi sikuwakuta nikajua wameenda nyumbani, sasa nikashangaa hawajafika ndio tukaanza kuwatafuta,” alisema Mayumba.

Alisema siku walipopatikana alianza kusikia harufu kali na akaona maji yakidondoka chini ya gari.

“Niliposikia harufu kali nilihisi panya amekufa au njiwa, nikaanza kutafuta ili nitoe, ghafla nikaona nzi wengi chini ya gari akili ikanituma nifungue mlango. Niliwakuta wajukuu zangu wakiwa wamekufa na mmoja alikuwa kichwa chini miguu juu,” alisema.

“Sipo sawa na sipendi sana kuongelea jambo hili kwa sababu linaliumiza, kila nikikumbuka moyo wangu unauma sana, sipo sawa.”

Hisia waliuawa

Mjomba wa watoto hao, Mohammed Mayumba alisema sio kweli kwamba watoto hao waliuawa.

“Hizi hisia tusizipatie nafasi hata kidogo, watoto wetu wamekufa na tayari polisi na hospitali walituambia walikosa hewa, ibaki hivyo. Sisi tunamshukuru sana Mungu,” alisema Mohammed.

Mohammed alisema tukio hilo linaacha funzo kwa wazazi na walezi kuwa makini na watoto.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Njaro, Amina Mlewa alisema miili ya watoto hao ilikuwa na viungo vyote.

“Lile gari hata sisi watu wazima tulipata tabu kufungua, mlango uliokuwa unafanya kazi ni mmoja tu,” alisema.

Alisema wakati wanatoa miili ya watoto hao ilibidi wavunje kioo cha nyuma.