‘Watekaji walitumia sekunde 30 kuondoka na mfanyabiashara Mo Dewji’

Muktasari:

  • Mfanyabiashara Mo Dewji alitekwa Alhamisi iliyopita alfajiri akiwa kwenye Hoteli ya Colosseum, Oysterbay, Dar es Salaam katika tukio lililochukua sekunde zisizozidi 30 na hadi sasa watu 26 wanashikiliwa na polisi.

Dar es Salaam. Ikiwa ni siku nne zimepita tangu kutekwa kwa mfanyabiashara maarufu nchini, Mohammed Dewji ‘Mo’ inadaiwa kuwa watekaji hao walitumia sekunde zisizozidi 30 kufanya tukio hilo.

Jambo jingine ambalo limefahamika ni kuwa makubaliano ya uwekezaji wa bilionea huyo na klabu ya Simba ni yake binafsi, hayana uhusiano wowote na kampuni anayoiongoza ya Mohammed Enterprises Limited (MeTL).

Mo alitekwa saa 11 alfajiri ya Alhamisi iliyopita katika Hoteli ya Colosseum, Oysterbay jijini Dar es Salaam na mpaka jana, watu 26 walikuwa wamekamatwa na polisi kwa ajili ya mahojiano.

Habari za ndani kutoka katika Hoteli ya Colosseum zinasema kuwa kamera za usalama (CCTV) zinaonyesha kuwa tukio lote la watekaji kumchukua Dewji na kumuingiza kwenya gari lao mpaka kujifungulia geti na kutokomea, lilichukua kati ya sekunde 20-30.

Inadaiwa kuwa watekaji walikuwa watatu, wawili walimshika aliposhuka kwenye gari lake na mwingine alifungua mlango wa gari na kusaidia kumpandisha kwenye gari lao.

Kwa mujibu wa maelezo ya polisi, kulikuwa na magari mawili yaliyoshiriki katika utekaji huo, moja lilikuwa limeegeshwa nje ya uzio na jingine lilikuwa ndani.

Polisi wanasema wakati gari la Mo lilipofika, gari la ndani liliwasha taa kuwapa ishara wenzao waliokuwa nje ambao waliingia na kuegesha karibu na gari la bilionea huyo kabla ya kumkamata aliposhuka na kumuingiza kwenye gari lao.

Watekaji hao walitokea katika geti jingine, baada ya kutofunguliwa geti hilo na mmoja wa watekaji aliteremka na kupiga risasi juu kabla ya kufungua mlango huo.

Wakati polisi wakisema kuwa watekaji wawili walikuwa ni Wazungu, habari za jana kutoka kwenye hoteli hiyo zinasema watu hao walikuwa wamejifunika nyuso zao na walikuwa wakizungumza Kiingereza.

Juzi, ikiwa imepita siku tatu tangu tukio hilo, Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola alizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam na kusema ndani ya miaka mitatu, watu 75 wametekwa nchini.

Aliwaambia wanahabari kuwa Mo Dewji ambaye miaka mitatu iliyopita Jarida la Forbes lilimtangaza kuwa tajiri namba 17 barani Afrika, alikuwa hajapatikana na kwamba upelelezi unaendelea.

Watu 26 wamekamatwa

Juzi, Lugola alisema watuhumiwa 20 walikuwa wametiwa nguvuni na Jeshi la Polisi kwa mahojiano kuhusiana na tukio hilo lakini mpaka jana sita waliongezeka.

Idadi hiyo mpya ilitangazwa na Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa akisema wengine sita wameongezeka.

Alisema Jeshi la Polisi litafika mahali popote ikiwamo hotelini, nyumbani na kuhoji kila mtu atakayeonekana anaweza kusaidia uchunguzi wa tukio la kutekwa Mo Dewji.

Alisema uchunguzi unaendelea na wataendelea kumchukua yeyote yule anayehitajika kwa ajili ya kusaidia shughuli za uchunguzi.

“Hadi jana (juzi) jioni walikuwa wamefika 26, lakini sina idadi ya leo (jana) kwa sasa,” alisema.

Siku ya tukio hilo, Jeshi la Polisi liliwakamata na kuwahoji watu 12 akiwamo msemaji wa klabu ya Simba, Haji Manara, wafanyakazi na walinzi wa hoteli hiyo.

Soma zaidi,

Hali ilivyo hoteli mbalimbali

Jana, waandishi wa gazeti hili walitembelea hoteli nne kubwa katika ufukwe wa Bahari ya Hindi na kuelezwa kuwa kuna mabadiliko ya ulinzi katika maeneo hayo tangu bilionea huyo kutekwa.

“Mabadiliko yapo polisi wameongezeka tofauti na ilivyokuwa hapo awali kabla ya tukio hilo,” alisema mmoja wa viongozi katika Hoteli ya Sea Cliff.

Meneja Mauzo wa Hoteli ya Golden Tulip, Mathias Marthias alisema hakuna mabadiliko yoyote kauli ambayo inafanana na iliyotolewa na Thomas Sambi wa Hoteli ya Serena.

Gari la Mo Dewji

Jana, waandishi wetu walifika katika Hoteli ya Colosseum na kukuta shughuli zikiendelea kama kawaida, lakini gari la mfanyabiashara huyo aina ya Range Rover ambalo alilitumia kufika hapo kabla ya kutekwa, halipo.

Alipoulizwa, Kamanda Mambosasa alisema gari hilo limehifadhiwa kama sehemu ya vielelezo.

“Baada ya kukamilisha upelelezi, vielelezo vinatunzwa na Jeshi la Polisi kwa hiyo kuondoka kwa gari wala siyo issue, ni kielelezo kile kimetunzwa.”

Kuhusu simu ya mfanyabiashara huyo, Mambosasa alisema hayo ni mambo ya upepelezi na asingependa kuyazungumzia. Jana saa nne asubuhi waandishi wetu walifika hotelini hapo na kuelezwa na mmoja wa maofisa kuwa polisi walifika na kumchukua mmoja wao.