Rais Magufuli aagiza vyombo husika kufanyia kazi mkasa mwanamke aliyeunguzwa

Rais John Magufuli

Muktasari:

Rais Magufuli ametoa agizo hilo baada ya kutoa pongezi kwa madaktari wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kwa juhudi kubwa walizofanya kunusuru maisha ya Neema ambaye alijeruhiwa kwa kuunguzwa na maji ya moto kifuani, shingoni na mkononi.

Dar es Salaam. Rais John Magufuli ameagiza vyombo vyote vinavyohusika kufanyia kazi mkasa uliomkuta Neema Mwita Wambura na kuhakikisha haki inatendeka.

Rais Magufuli ametoa agizo hilo baada ya kutoa pongezi kwa madaktari wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kwa juhudi kubwa walizofanya kunusuru maisha ya Neema ambaye alijeruhiwa kwa kuunguzwa na maji ya moto kifuani, shingoni na mkononi.

Kabla ya kutoa pongezi hizo, mapema leo (Alhamisi) asubuhi Rais Magufuli amewatuma wasaidizi wake wakiongozwa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu Gerson Msigwa kwenda Tandika Devis Kona katika Wilaya ya Temeke Jijini Dar es Salaam kumuona Neema ambaye alipatiwa hifadhi katika nyumba ya Mama Mjane aitwaye Mariam Amir (Bibi Mwanja) baada ya kuona picha na kusoma taarifa za mkasa uliomkuta katika mitandao ya kijamii.

Rais Magufuli ametoa Sh 500,000  kwa Neema kwa ajili ya kumsaidia chakula yeye na watoto wake waliohifadhiwa na rafiki yake huko Bunda Mkoani Mara na pia ametoa Sh 500,000 Mariam Amir aliyejitolea kumsaidia na kumpa hifadhi nyumbani kwake.

Pia ameahidi kumsaidia wakati wote wa matibabu na pia familia yake.